Stori: Waandishi Wetu SIKU chache baada ya kufunga ndoa, Rais wa Bendi ya Mashujaa Musica, Charles Gabriel Baba ‘Chaz Baba’ ameingia kwenye mateso ya kusumbuliwa na madeni yaliyotokana na harusi hiyo.Akizungumza na mapaparazi wa Amani katika mahojiano maalumu yalifofanyika nyumbani kwake Mwananyamala jijini Dar hivi karibuni, Chaz Baba alisema baadhi ya wanakamati wasiokuwa waaminifu walichakachua michango na kusababisha deni limuangukie yeye. “Yaani harusi ilipokwisha tu, nilijikuta nikidaiwa karibu shilingi milioni 6 ambayo kimsingi wanakamati walizichikichia na mimi nikalazimika kudaiwa na wahusika wa ukumbi na mambo mengine kibao,” alisema Chaz Baba. Akiendelea kushusha malalamiko yake kwa wanakamati hao, Chaz Baba alikwenda mbali zaidi na kusema imefika wakati hata ndoa anaiona chungu kwani madeni hayo yanamweka katika msongo wa mawazo kusaka suluhu. “Ndoa naiona chungu, mke wangu mjamzito, kodi ya nyumba inakaribia kuisha. Kutokana na kuandamwa na madeni yaliyosababishwa na watu niliowaamini, natamani hata nimrudishe mke wangu kwao kwa muda,” alisema Chaz. Alipoulizwa kama amewahi kujaribu kuwahoji wanakamati hao anaodai wamechikichia fedha za michango, Chaz alisema amewahi lakini hawakumpa msaada wala dalili za kurejesha fedha hizo. “Nimeongea nao na wengine waliniahidi kuwa watazirejesha fedha hizo na wengine kuahidi kuwa watanisaidia kulipa deni lakini hadi sasa sioni chochote kinachoendelea,” alisema Chaz. Kwenye deni hilo la shilingi milioni 6, hadi sasa Chaz Baba amejitutumua kupunguza na kubakisha deni la shilingi milioni nne na laki saba.
Habari imeandikwa na Shakoor Jongo na Musa Mateja. |
0 Comments