Aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor atatumikia kifungo chake cha miaka 50 jela nchini Uingereza baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa kivita.Haya ameyasema waziri wa sheria nchini Uingereza Jeremy Wright.Sweden na Rwanda pia zilikuwa zimeomba kumfunga jela Taylor katika ardhi yao baada ya rufaa yake kukataliwa na mahakama mwezi jana.Taylor alihukumiwa kifungo cha miaka 50 jela na mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu Sierra Leone, mjini Hague.
Iliamua kuwa makosa dhidi yake yalithibtishwa bila tashwishi.
Alihukumiwa jela mwaka 2012 kwa kuwasidia waasi waliofanya maasi makubwa dhidi ya watu wa Sierra Leone wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Taylor, mwenye umri wa miaka 65, alipatikana na hatia ya kuwapa waasi wa Revolutionary United Front silaha na wao wakimpa almasi kutoka Sierra Leone.