Zeidan alitoa wito kwa Marekani kusaidia Libya kupambana na
wapiganaji wa kiisilamu
Waziri mkuu wa Libya Ali Zeidan aliyeripotiwa kutekwa nyara na
waliokuwa waasi katika jiji kuu la Libya Tripoli mapema hivi leo
ameachiliwa.
Maafisa wamenukuliwa wakisema kuwa hakuumizwa. Tukio hilo limeshutumiwa na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William
Hague. Ali Zeidan alitekwa nyara na kundi la waasi waliokuwa na uhusiano na serikali
kwa jina Revolutionaries Operations Room. Walisema walimteka nyara kwa maagizo ya mwendesha mkuu wa mashitaka ingawa
wizara ya sheria imekanusha madai hayo. Kundi hilo lilikuwa miongoni mwa makundi ya wapiganaji walioghadhabishwa na
hatua ya makomando wa Marekani kumkamata Anas Al-Liby mshukiwa wa kundi la
kigaidi la al-Qaeda . Wengi walitaja hatua ya Marekani kama ya kuingilia uhuru wa taifa hilo na
hata kutaka maelezo kutoka kwa balozi wa Marekani nchini humo. Mwandishi wa BBC mjini humo anasema Zeidan alitekwa nyara akiwa ndani ya
hoteli ya kifahari anamoishi. Serikali imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kali baada ya makomando wa Marekani
kumkamata mmoja wa viongozi wa al-Qaeda Anas al-Liby nchini Libya. Bwana Liby alikamatwa Jumamosi mjini Tripoli kwa madai ya kuhusika na
mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya balozi za Marekani nchini Tanzania
na Kenya mwaka 2008. Mnamo siku ya Jumatatu Libya ilimhoji balozi wa Marekani kuhusu kukamatwa Al
Liby. Kwa upande wake Zeidan alitoa wito kwa Marekani na nchi za Magharibi
kuisaidia serikali ya Libya kukomesha vitendo vya wapiganaji wenye itikadi kali
nchini humo. Kwenye mahojiano na BBC, alisema kuwa Libya inatumiwa kama kambi ya kuweka
silaha. Waziri mkuu aliambia BBC kuwa nchi yake inatumia kama kivukio cha
kusafirishia silaha kwenda katika maeneo mengine ya kanda hiyo.
0 Comments