Kumekuchaaaaa!!!Hayawi hayawi sasa yamekua!! Young Africans mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom leo wamekamata usukani wa kiti cha uongozi baada ya kuichapa timu ya JKT Oljoro kwa mabao 3 - 0 katika mchezo uliofanyika dimba la uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Baada ya mchezo wa leo wapenzi, washabiki na wanachama wa Young Africans waliamsha shangwe uwanjani kufutia kupata matokeo ya timu za Mbeya City na Azam ambao walikuwa wakiongonza Ligi kwa muda mrefu kutoka sare ya mabao 3-3.
Kwa matokeo hayo ya leo Young Africans imefikisha pointi 28 na mabao 31 ya kufunga huku Azam ikifuatia kwa pointi 27 sawa na Mbeya City wakiwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na Simba SC wakishika nafasi ya nne kwa kuwa na pointi 24.
Ikicheza soka safi na la kuvutia Young Africans ilianza mchezo kwa kasi kwa lengo la kusaka bao la mapema ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuongoza Ligi na ndivyo ilivyokua kwa vijana wa jangwani kupeleka furaha na shangwe kwa washabiki wake.
Saimon Msuva aliipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 23 ya mchezo kwa kichwa akiunganisha vizuri krosi ya kiungo mnyarandwa Haruna Niyonzima aliyewatoka walinzi wa JKT Oljoro na kuukwamisha mpira wavuni.
Mara baada ya bao JKT Oljoro waliendelea kujikanyaga wenyewe na al-manusra Hamis Kiiza aipatie timu yake bao dakika ya 26 ya mchezo baada ya mpira alioupiga kuokolewa na walinzi wa Oljoro na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Dakika ya 30 Mrisho Ngassa aliipatia Young Africans bao la pili kwa jitihada binafsi baada ya kuukokota mpira kuanzia kati kati ya uwanja na kufumua shuti kali la umbali wa mita 25 na kutinga wavuni moja kwa moja na kuongeza shangwe kwa washabiki wa Young Africans.
Mpaka ulikwenda mapumziko, Young Africans 2 - 0 JKT Oljoro.
Kipindi cha pili cha mchezo kilianza kwa kocha mkuu Ernie Brandts kufanya mabadiliko ambapo alimtoa Hamis Kiiza na nafasi yake kuchukuliwa na Jerson Tegete ambaye aliongeza nguvu na uwezo wa kumiliki mpira.
Dakika ya 54, Jerson Tegete aliipatia Young Africans bao la tatu na la ushindi baada ya krosi iliyopigwa na Mrisho Ngassa kumkuta Tegete ambaye aliukwamisha mpira wavuni na kuendeleza furaha kwa washabiki wake.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 3 - 0 JKT Oljoro.
Mara baada ya mchezo wa leo, kocha Brandts ametoa mapumziko ya wiki kwa wachezaji wake kufuatia wengi kujiunga na timu za Taifa na kikosi kinatarajiwa kuanza mazoezi tena Novemba 24, 2013 kujiandaa na mzunguko wa pili na mashindano ya kimataifa.
Young Africans: 1.Dida, 2.Twite, 3.Oscar, 4.Cannavaro 5.Yondani, 6.Chuji 7.Msuva 8.Domayo, 9.Kiiza/Tegete,10.Ngassa, 11.Niyonzima/Lusajo
|
0 Comments