Rais Kikwete akilihutubia Bunge.PICHA|MAKTABA 
Dodoma.
Wabunge wamempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kutoa hotuba ambayo imetoa msimamo wa Serikali kuhusiana na kitendo cha Tanzania kutengwa na baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Wakizungumza muda mfupi mara baada ya Rais Kikwete kulihutubia Bunge jana, baadhi ya wabunge walisema ni vizuri Rais akapanga utaratibu wa kutolea ufafanuzi masuala yanayolihusu Taifa.
“Hotuba yake imekuwa wazi na imeonyesha msimamo wa nchi yetu ya kwamba itifaki ya makubaliano ya EAC ni lazima iende hatua kwa hatua,” alisema Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema), Said Arfi.
Hata hivyo, alisema Watanzania walitaka kujua mambo zaidi ya hayo kwa kuwa hivi sasa suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki ni miongoni mwa matatizo yanayolikabili Taifa.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ritta Kabati alisema wabunge wengi sasa wameelewa mambo mbalimbali kutokana na hotuba hiyo.
“Sisi Wabunge tumekuwa tukilalamikia majibu yanayotolewa na mawaziri kuhusiana na hoja mbalimbali lakini hapa sasa imetuwezesha kujua msimamo wa nchi katika suala hili nini,” alisema.
Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba alisema hotuba hiyo ilijaa hekima na imekidhi haja.
“Hotuba hii imetoa mwelekeo wa nchi, yeye ni `President (Rais)’ na ndiyo kazi yake,” alisema Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara).
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alisema hotuba ya Rais imekata kiu ya wabunge.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Mosses Machali alisema: “Ilikuwa ni nzuri, ametumia diplomasia kubwa katika kueleza masuala ya EAC ingawa amegusia vitu vichache sana.”
Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa alisema hotuba hiyo imesaidia kutoa msimamo wa Tanzania katika suala la jumuiya hiyo.
“Sote tumemwona alivyokuwa akizungumza kwa hisia na masikitiko kuhusiana na hali ilivyo katika jumuiya hiyo,” alisema.Alisema jambo la msingi ni wanachama wa jumuiya hiyo kufahamu kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Katika siku za karibuni nchi za Kenya, Rwanda na Uganda zimekuwa zikifanya vikao nje ya EAC na kuzitenga Tanzania na Burundi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta wamekaririwa kwa nyakati tofauti wakilalamikia hatua ya Tanzania kutengwa bila kutoa msimamo wa Tanzania kuhusu hatua hiyo.