Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akijibu maswali ya waandishi wa habari jana alipokutana nao Ikulu mjini Zanzibar. Picha na Martin Kabemba 

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema hakuna kiongozi yeyote wa Zanzibar mwenye mamlaka ya kuzungumzia msimamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuhusu masuala ya Katiba na Muungano isipokuwa yeye na kwamba kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad ni zake binafsi au za chama chake.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Zanzibar jana juu ya tathmini ya uongozi wa Awamu ya Saba anayoiongoza, Dk Shein alisema kuna changamoto kubwa za kuendesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kwamba jambo muhimu ni kuvumiliana.
Tangu kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya, msimamo wa Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, umekuwa ni kuundwa kwa Serikali Tatu au ya Mkataba, ambao unapingana na ule wa CCM, wa kutaka Serikali mbili kama ilivyo sasa.
Rasimu ya kwanza iliyotolewa na Tume ya Marekebisho ya Sheria imependekeza kuwapo kwa Serikali Tatu, ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar.
“Serikali yangu haina msimamo wa jambo hilo. Kila mwananchi ana uhuru wa kutoa maoni yake, ninaweza kutoa msimamo kutokana yaliofikiwa na uamuzi wa chama changu na kila mtu anaweza kufanya hivyo na si kuisemea Zanzibar na wananachi wake.”
Alimsifu Rais Jakaya Kikwete kwa dhamira yake ya kusimamia suala la mabadiliko ya Katiba na mchakato ulivyokwenda na sasa taifa linaelekea kupata Bunge la Katiba kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni mwakani.
Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Dk Shein alisema imefanikiwa kudumu kwa miaka mitatu sasa kutokana na kuvumiliana na kufanya kazi kwa pamoja bila ya kutanguliza itikadi za kisiasa. “Nchi nyingi zimejaribu hili zimeshindwa, lakini sisi tumefanikiwa kwa sababu tunavumiliana. Hili linahitaji stahimili kubwa vinginevyo tutagawana mbao na sitaki hili litokee kwenye uongozi wangu.”
Akizungumzia masuala ya Muungano, Dk Shein alisema licha ya mchakato wa Katiba Mpya kuendelea, Serikali zote mbili (Muungano na Zanzibar), zimeendelea kujadili masuala muhimu na changamoto zilizopo na kusema siyo sahihi kubeza mgawo wa sasa wa mapato ya Muungano ambao Zanzibar inapata asilimia 4.5.
“Jeshi la Wananchi na JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) wanatumia mabilioni mangapi, Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani, Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia... Sisi (Zanzibar tunatoa ngapi?)”
Uchumi
Akizungumzia ukuaji wa uchumi katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, Dk Shein alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la ukusanyaji wa mapato akisema katika mwaka wa fedha wa 2010/11 Sh181.4 bilioni zilikusanywa na mwaka uliofuata wa 2011/12 makusanyo yaliongezeka hadi kufikia Sh212 bilioni na mwaka wa fedha wa 2012/13 kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia Sh266. 2 bilioni.
Alisema uchumi wa Zanzibar umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka. Alisema mwaka 2010 uchumi ulikua kwa asilimia 6.4, mwaka 2011 asilimia 6.7, mwaka 2012 asilimia saba na mwaka huu unatarajiwa kukua hadi kufikia asilimia 7.5.Alisema mchakato wa ujenzi wa Kiwanda cha Maziwa Fumba upo katika hatua nzuri na kitakapokamilika kitakuwa cha aina yake Afrika Mashariki na kitaajiri watu 200. Aidha, Kiwanda cha Sukari Mahonda nacho kinakaribia kuanza uzalishaji na kitaajiri watu 350.
Kuhusu utalii, Dk Shein alisema Serikali yake imedhamiria kuimarisha sekta hiyo muhimu kwa uchumi wake na moja ya mikakati ni kuwa na vijiji maalumu vya utalii, baada ya kile cha Nungwi ambacho kilikuwa cha mfano kuonyesha mafanikio makubwa.
Hata hivyo, alisema sekta hiyo inahitaji uwekezaji mkubwa na kutoa mfano wa Shelisheli ambayo inawekeza Dola za Marekani 9 milioni kwa mwaka kuutangaza utalii wake, Kenya Dola 4 milioni Tanzania Bara Dola 4 milioni wakati Zanzibar inawezeka Dola 250,000.
Akizungumzia umeme, Rais huyo wa Saba wa Zanzibar alisema katika kipindi cha miaka mitatu tayari vijiji 110 vimeshapatiwa huduma hiyo kati ya hivyo 65 vya Unguja na 45 vya Pemba na kwamba huduma hiyo ya nishati imeshasambazwa visiwani humo kwa asilimia 87.5... “bado asilimia 12.5 kukamilisha kazi hiyo.”
Usafiri wa Bahari
Akizungumzia usafiri wa bahari, Rais Shein alisema Serikali imeagiza meli kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 200 za mizigo pamoja na nyingine ya mafuta ambazo zote zinatarajiwa kuwasili nchini Juni 2015.