Dar es Salaam. Majiji yote matano nchini pamoja na Zanzibar na mikoa mingine kadhaa yatakuwa na giza kwa siku kumi kuanzia leo, hivyo kusababisha adha kwa wakazi wake. 
Meneja Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Badra Masoud, amethibitisha kuwepo kwa adha hiyo, akielezea kuwa hali hiyo inatokana na kuzimwa kwa mitambo ya Kampuni ya Pan African iliyopo Songosongo.
“Mitambo hiyo itazimwa kwa sababu ya matengenezo ya lazima, hakuna jinsi ya kuzuia hali hiyo Tanesco tunasikitika sana kwa kuwa kutakuwa na upungufu mkubwa wa umeme kwenye gridi ya taifa,” alisema Masoud.
Alifafanua mitambo hiyo inaendeshwa na gesi ambayo imepungua katika kisiwa hicho cha Songosongo Wilaya ya Kilwa, Lindi. 
“Upungufu huo umesababishwa na matengenezo ya kiufundi yanayofanywa kwenye visima vya gesi, lengo ni kuboresha upatikanaji wa gesi ya kutosha kwenye visima hivyo,” alisema.