Askari Kanzu wakikagua magunia yenye meno ya Tembo yaliyokuwa yamehifadhiwa katika Kontena la futi 40 yakiwa katika mpango wa kusafirishwa nje ya nchi katika bandari ya Malindi Zanzibar. PICHA | MWINYI SADALLAH
Zanzibar. Maofisa wawili waandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar wamekamatwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na mtandao wa usafirishaji wa magendo ya meno ya tembo yaliyokamatwa Bandari ya Malindi, Zanzibar.
Kukamatwa kwa watu hao kunafanya idadi yao kufikia wanne.
Akizungumza na gazeti hili, Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema maafisa hao wamekamatwa na watafunguliwa mashtaka yao Tanzania Bara kutokana na Zanzibar kutokuwa na Sheria ya Nyara za Serikali.
Maofisa waliotiwa nguvuni ni Mohamed Hija Mashaka na Omar Hamad Omar wote ni maofisa wa TRA kituo cha Bandari Malindi mjini Unguja wenye dhamana ya uhakiki na usafirishaji wa mizigo nje ya nchi.
“Watafunguliwa mashkata Bara kwa vile Zanzibar hakuna sheria ya nyara za Serikali,” alisema Mussa na kuongeza uchunguzi bado unaendelea.
Hata hivyo, alisema kampuni iliyokuwa ikisafirisha mzigo huo ya Island Sea Shells imebainika kuwa haina ofisi na wala anuani zake hazifahamiki.
“Tumefuatilia kwa Msajili wa Kampuni Zanzibar, hatukuona jina la kama hilo,” alisema Kamanda Mussa.
“Hii ni kampuni ya mifukoni (briefcase company), ingawa kuna majina ya watu waliosajili kampuni hiyo.”