Dar es Salaam.
Siku moja baada ya wabunge kuwataka Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili, pembe 706 za ndovu zimekamatwa jijini Dar es Salaam.
Pembe hizo 706 ni sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi za wanyama pori mbalimbali hapa nchini. Tukio hilo lililotokea jana jioni katika Mtaa wa Kifaru, Mikocheni, wilayani Kinondoni, liliongozwa na Waziri Kagasheki ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tarish Maimuna.
Waliokamatwa na shehena hiyo ya pembe za ndovu ni raia watatu wa China ambao ni Xu Fujie, Chen Jinzha na Huang Qin wote kutoka mji wa Guandung .
Raia hao wa China wamekuwa wakiishi katika nyumba hiyo kwa miaka mingi wakifanya biashara ya kuingiza nchini vitunguu swaumu kutoka China na kusafirisha nje ya nchi makombe yanayopatikana baharini.
Alipoingia ndani ya nyumba hiyo, Kagasheki ambaye aliambatana na askari polisi na baadhi ya maofisa usalama alishuhudia shehena kubwa ya pembe za ndovu ikiwa imehifadhiwa kwenye viroba vyenye uzito wa kilo 50.
Mbali ya kushuhudia shehena ya pembe hizo, alionyeshwa gari maalumu aina ya Toyota Noah ambalo watuhumiwa hao hulitumia kutoa pembe porini na kuyaingiza jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika eneo la tukio mara baada ya kuwakamata alisema kukamatwa kwa watu hao kunatokana na matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo imesitishwa na Serikali juzi baada ya wabunge kuilalamikia.
Waziri Kagasheki alisema kwamba katika harakati za kutaka kuwakamata watuhumiwa hao walitoa Sh30 milioni kwa ajili ya kujaribu kuwahonga askari.
“Walitaka kuwahonga askari ili wasikamatwe,” alisema huku akionyesha noti za fedha hizo.
Alisema wabunge wanaomtaka ajiuzulu kwa madai kwamba Operesheni Tokomeza Ujangili imesababisha mauaji ya watu na mifugo wanapoteza muda kwa kuwa mwenye mamlaka ya kumtoa ni Rais Jakaya Kikwete pekee.
“Sasa mimi nasema kunitoa haitakuwa rahisi anayeweza kunitoa ni yule aliyeniweka,” alisema.
Alisema ipo mikakati inayofanywa na baadhi ya wabunge kutaka kuwang’oa baadhi ya mawaziri kwa masilahi binafsi ya kisiasa.“Itakuwa ni jambo la ajabu kwamba kila mtu akiingia madarakani wanataka atoke, watatolewa wangapi?” alihoji na kuongeza kuwa operesheni hiyo ni muhimu kwa ajili ya kunusuru tembo wasiishe.
Alisema kwamba ni kweli kuna baadhi ya dosari zimejitokeza kwenye operesheni ikiwamo kuuawa kwa baadhi ya mifugo, lakini siyo kwamba zoezi zima halina manufaa.
Kagasheki alisema kama kasi hii ya kuuawa kwa tembo itaachiwa iendelee baada ya miaka 10 tembo wote watakuwa wameisha nchini.
Alisema hataki kuona utawala wa Rais Kikwete ukiondoka madarakani ukiwa na lawama ya kuachia majangili wawamalize tembo.
Mmoja wa watuhumiwa hao, Huang Qin alisema shehena yote ya pembe za ndovu iliyokamatwa nyumbani kwake ilikuwa ikiletwa kidogo kidogo na rafiki yake ambaye hakumtaja jina.
Akiongea kwa Kiswahili Qin alisema: “Mimi hii si yangu, kichwa yangu mbovu. Rafiki yangu alileta hii (pembe) kidogo kidogo.”
Januari mwaka huu, Gazeti La Daily Mail la Uingereza liliripoti kwamba Serikali ya Kenya imekamata shehena ya vipande 638 vya pembe za ndovu ambavyo ni sawa tembo 320 waliouawa.
Mzigo huo wa tani mbili ulikuwa kwenye kontena la mawe ya urembo (marumaru) kutoka Tanzania.
Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa tani nne za pembe za ndovu zenye thamani ya Dola za Marekani 3.4 milioni sawa na takriban Sh5.4 bilioni zilikamatwa Hong Kong Oktoba 20, mwaka jana, huku ikielezwa kuwa meno hayo yalikamatwa yakisafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.
Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia wa Vietnam akiwa na pembe za ndovu yenye thamani ya Sh18.4 milioni yaliyotengenezwa kama bangili tayari kusafirisha kwenda nje ya nchi.
0 Comments