Wachezaji wa Yanga wakishangilia baada ya mshambuliaji Jerryson Tegete kufunga bao la nne dhidi ya JKT Ruvu jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga ilishinda 4-0. Picha na Michael Matemanga
Dar es Salaam. Mabingwa watetezi, Yanga wamekwea kileleni mwa Ligi Kuu Bara baada ya kuichakaza JKT Ruvu mabao 4-0 jana  kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Mrisho Ngassa aliifungia mabao mawili ya haraka dakika 3 na 10 kabla ya Oscar Joshua (46) na Jerryson Tegete (88) kuhakikishia Yanga kukalia usukani wa Ligi Kuu kwa pointi 25, kabla ya mechi za leo za Azam na Mbeya City.
Ngassa alifunga bao la kwanza kwa shuti la umbali wa meta 25, lililomwacha kipa wa JKT Ruvu, Sadick Mecks asijue la kufanya.
Jahazi la maafande wa Ruvu lilizidi kwenda mrama dakika 13 baada ya Ngassa kuunganisha kwa kichwa mpira wa kurusha wa Mbuyu Twite na kuifungia Yanga bao la pili.
Yanga walitawala zaidi sehemu ya kiungo ikiwa chini ya mkongwe Athuman Idd, Frank Domayo na Ngassa waliokuwa wakifanya wapendavyo katikati ya uwanja.
Beki Joshua alifunga bao lake la kwanza msimu huu dakika 46, baada ya mabeki wa JKT Ruvu kushindwa kuokoa hatari golini kwao.
Bao hilo la Joshua lilishangiliwa kwa nguvu na wachezaji na mashabiki wa Yanga waliojitokeza uwanjani hapo.
Mshambuliaji Hamis Kiiza alikosa bao dakika 56, baada ya kushindwa kumalizia krosi nzuri ya Jabu Msuva akiwa yeye na goli.
Tegete aliyeingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya Didier Kavumbagu alifungia Yanga bao la nne dakika 88 akimalizia vizuri krosi ya Msuva.
Katika hatua nyingine, raundi ya 12 ya ligi hiyo itaendelea leo
kwa mitanange minne itakayotimua vumbi kwenye miji minne tofauti.
Azam watakuwa kwenye uwanja wao wa Azam Complex kuwakaribisha Ruvu Shooting, wakati Mbeya City watakuwa nyumbani Sokoine kupepetana na Ashanti United.
Azam na City kama zitashinda mechi zao wataishusha Yanga hadi nafasi ya tatu.
Mechi nyingine itakuwa jijini Tanga, Mgambo Shooting inayokamata mkia itapimana ubavu na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, huku Mtibwa Sugar ikivaana na Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Vikosi
JKT Ruvu: Sadick Mecks, Musa Zuberi, Kessy Mapande, Omari Mtaki, Damas Makwaya, Nashon Naftal, Amos Mgisa, Haruna Adolf, Paul Ndauka, Samwel Kamutu na Sosthenes Manyasi.
Yanga: Deogratius Munishi, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza