Clement Mabina hivi karibuni alienguliwa kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Anthony Diallo baada ya kushindwa kwa wingi wa kura.
Mwanza. 
Mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina ameuawa na wananchi wenye hasira baada ya kuzuka mgogoro wa ardhi baina yao.
Mabina aliuawa katika Kata ya Kisesa, baada ya wananchi wenye hasira kumtuhumu kumuua kwa kumpiga risasi mmoja wa wakazi wa eneo hilo.
Jina la mkazi aliyepigwa risasi halikupatikana na kwamba alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali kwa matibabu.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Joyce Masunga alithibitisha kuuawa kwa Mabina, ambaye miezi ya karibuni alikuwa ni mwenyekiti wake.
Jinsi alivyouawa:
Masunga alisema taarifa zilizomfikia zinaeleza kuwa Mabina alijikuta anaingia kwenye mgogoro na wananchi hao saa 11:00 asubuhi.
Alisema mgogoro huo ulianza wakati kundi la watu waliotumwa na Mabina walipoanza kuweka alama za mipaka kwenye shamba linalodaiwa kumegwa kwenye eneo la wakazi hao.
Wakazi hao walipopata taarifa hizo, walijitokeza kuzuia kundi hilo lisitekeleze kazi hiyo.
Kundi hilo lilipopata upinzani huo, liliwasiliana na Mabina kumweleza kwamba wamezuiwa kufanya kazi aliyowaagiza.
Inadaiwa kuwa Mabina kusikia hivyo, aliharakisha kwenda eneo hilo ili kujaribu kusuluhisha mgogoro huo ili maelekezo yake yafanyike kama alivyopanga.
Miongoni mwa watu waliokuwa kwenye eneo hilo, alisema wakati wanajibizana na wananchi hao, Mabina alimpiga risasi mmoja wa wakazi hao na kuanguka chini.
Walieleza kuwa tukio hilo liliwapandisha hasira wakazi hao na kusababisha wamshambulie kwa kumrushia mawe, vipande vya miti na silaha mbalimbali kwa kadri kila mmoja alivyoweza.Hali hiyo, wanaielezea ilisababisha kuanguka chini na wakazidi kumshambulia hadi wakahakikisha amekufa huku vijana wake wa kazi wakiingia mitini.
Ofisa wa Polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa yeye si msemaji wa jeshi hilo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Taarifa hiyo ya polisi ilieleza kwamba, mgogoro huo ulizuka baada ya wananchi hao kumtuhumu Mabina kuwa ana mpango wa kuuza eneo lao la kijiji kwa mwekezaji.
“Ni mapema mno kuelezea tukio hili kwa undani hasa ikizingatiwa kuwa mimi siyo msemaji. Subiri msemaji wa jeshi atawapa taarifa kwa undani,” alisema ofisa huyo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Christopher Fuime alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema wanaendelea kufanya uchunguzi.”
“Tulipata taarifa ya kuwepo kwa tukio hilo na kutuma vijana wetu kwenda kutuliza vurugu,” alisema Fuime. Alisema Mabina hakuwa na dhamira ya kuua, ila alijaribu kufyatua risasi hewani kwa lengo la kuwatuliza na ndipo ilipompata mmoja wao.