Shamsi Vuai Nahodha
Dodoma.
Kamati ya Bunge ya kuchunguza athari za Operesheni Tokomeza Ujangili inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake leo, ambayo inaelezwa kuwa imependekeza kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya vigogo kadhaa wa Serikali.
Taarifa ya kamati hiyo ndogo itasomwa leo wakati Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili itakapokuwa inawasilisha taarifa yake ya utendaji kazi bungeni.
Wajumbe wengi wa kamati hiyo ndogo wanatokana na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili. Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ya uchunguzi alimdokeza mwandishi wetu jana kuwa uchunguzi wa kamati hiyo umegundua udhaifu mkubwa katika wizara na idara za Serikali.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli imependekeza kuchukuliwa hatua kwa baadhi ya maofisa waandamizi wa Wizara za Maliasili na Utalii na Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Mjumbe huyo alisema kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii, watakaoguswa na ripoti hiyo ni baadhi ya maofisa waandamizi wanaosimamia wanyamapori na hata wale wa maliasili.
Kamati hiyo iliyoanza kazi Novemba 25, mwaka huu inawasilisha ripoti yake baada ya kumaliza kazi ya kuwahoji watu mbalimbali wakiwamo mawaziri watatu ambao wizara zao zilihusika moja kwa moja na operesheni hiyo.
Mawaziri waliohojiwa katika Hoteli ya Bahari Beach, Dar es Salaam ni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emanuel Nchimbi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana jana zilisema kuna uwezekano mkubwa taarifa hiyo ‘ikamkaanga’ Dk Mathayo kutokana na mapendekezo ya wabunge katika mkutano wa 13.
Wabunge walikerwa zaidi na kauli ya Dk Mathayo alipopata fursa ya kuchangia taarifa ya Serikali kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili na kuishia kuwapa pole wafugaji ambao mifugo yao iliuawa kwa risasi.
Katika operesheni hiyo, wabunge walipaza sauti wakidai wapo raia wasio na hatia waliouawa na kuteswa, huku mifugo ikiporwa na mingine kama ng’ombe ikiuawa kwa kupigwa risasi.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola ndiye aliyekuwa mwiba kwa mawaziri hao aliposema ana kitabu kilichosheheni ushahidi dhidi ya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu. Habari zaidi zinasema kamati hiyo ya uchunguzi imelazimika kutofanyia shughuli zake katika kumbi za Bunge ili kukwepa vishawishi kutoka kwa watu wa karibu na vigogo wanaotuhumiwa.
“Wamejificha katika hoteli moja tangu waliporudi Dodoma wiki iliyopita ili kuandaa ripoti yao kwa sababu hawataki kuingiliwa ingiliwa na hili ndilo linalowatia hofu mawaziri,” alisema mjumbe huyo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, pamoja na kasoro za operesheni hiyo, ilisaidia kuwabaini maofisa walioko katika mtandao wa ujangili na baadhi yao walikamatwa na nyara za Serikali.Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alithibitisha kuwasilishwa kwa ripoti hiyo leo wakati kamati itakapowasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli zake... Hata hivyo, alisema hana uhakika wa asilimia 100. Ripoti hiyo itawasilishwa huku kukiwa na vuguvugu la kung’olewa kwa mawaziri saba wanaodaiwa mzigo katika utendaji wao na tayari wamehojiwa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi iliyokutana wiki iliyopita chini ya Mwenyekiti wake, Rais Kikwete.
Mbali na vuguvugu hilo, ripoti ya uchunguzi pia inawasilishwa wakati tayari Bunge limepitisha azimio la kuwataka mawaziri watatu wajipime kama bado wanatosha kuongoza Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Mawaziri hao ni Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na Manaibu wake, Aggrey Mwanry na Kassim Majaliwa. Ripoti kama hiyo inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo na Lembeli ndiyo iliyochangia kumng’oa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige kutokana na kashfa ya ugawaji vitalu vya uwindaji.
                                                                     CHANZO CHA HABARI