Na Mashaka Baltazar, Mwanza
MAMBO mazito yameibuka baada ya kifo cha kigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Diwani wa Kata  ya Kisesa, Clement Mabina jijini Mwanza  kwa mwanasiasa mmoja kutajwa kuhusika na mauaji hayo, Risasi Mchanganyiko limeambiwa.

Clement Mabina enzi za uhai wake.
Habari zilizosambaa jijini hapa zinadai kwamba  mwanasiasa huyo (jina kapuni) andaiwa kuwagawia fedha baadhi ya wanakijiji waliohusika ili  kukatisha uhai wa Mabina.
“Hakuna asiyejua kwamba jambo hili lina mkono wa kisiasa ndani yake, mapema kabla ya marehemu kwenda Kanyama kwenye eneo la tukio mmoja wa wanasiasa mashuhuri alipita na kuwashawishi wanakijiji wasikubaliane na hoja zake na ikiwezekana wammalize,” alisema mmoja wa watu waliokuwa wakizungumzia kifo cha Mabina.

Mwili wa Mabina baada ya kushambuliwa.
Hata hivyo, polisi wanawashikilia watu saba wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo ya kinyama.
Kamanda wa Polisi wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, SACP, Valentino Mulowola, akizungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu, alisema hadi sasa watu saba wanashikiliwa na jeshi hilo.

Kamanda alisema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti jana ambapo jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika katika mauaji ya  diwani huyo ambaye zamani alikuwa ni mwenyekiti CCM Mkoa wa Mwanza.
Katika tukio hilo la mauaji, Mabina aliuawa kwa kukatwa mapanga na kupigwa mawe ambapo alikutwa na majereha makubwa kichwani sehemu za kisogoni.
Kabla ya kuawa na wananchi  hao, marehemu alimpiga risasi mtoto Temeli Malemi (11) kwa  bahati mbaya wakati akijihami na mashambulizi ya wananchi hao.
Imeelezwa na Kamanda wa Polisi SACP Mulowola kuwa marehemu alikutwa na silaha mbili aina ya Short-gun na bastola moja.
Hata hivyo ndugu wa marehemu walishindwa kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kuhusiana na habari zilizoandikwa na mitandao ya kijamii kuhusisha kifo cha ndugu yao (Mabina) na masuala ya kisiasa.
Aidha habari kutoka eneo la tukio zainadai kuwa mmoja wa watuhumiwa alikamatwa na simu ya mkononi ya marehemu,hata hivyo kamanda hakutaka kutaja majina  ya watuhumiwa hao kuhofia kuvuruga upelelezi.