Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Dar es Salaam.
 Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu amesema atazungumzia hatima yake baada ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Gazeti  la The Citizen, lilimkariri Pinda jana akisema kwa sasa anahitaji amani na utulivu katika kipindi hiki cha sikukuu baada ya shughuli za kikao kilichopita cha Bunge.
Katika kikao hicho, mawaziri wannewalitimuliwa baada ya ripoti ya kamati ndogo ya Bunge kufichua madhara yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Wabunge kadhaa walishinikiza kujiuzulu kwa Pinda na mawaziri wengine, ambao wizara zao zilihusika katika utekelezaji wa operesheni hiyo.
“Baada ya kikao cha Bunge Dodoma nilikwenda likizo kuwasalimia wazazi wangu. Wasiliana na mimi baada ya likizo halafu niulize maswali yako yote nitakujibu,” alisema Pinda, ambaye yuko katika Kijiji cha Kibaoni, Mkoa wa Katavi.
Rais Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wa mawaziri Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk David Mathayo(Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo), baada ya malalamiko ya wabunge.
Pinda alikiri bungeni kuwa operesheni hiyo ilikuwa na matatizo na wale wote waliokuwa na dhamana walikiuka taratibu za utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Pamoja na kujiuzulu kwa mawaziri hao, pia Serikali itaunda tume, ambayo itaongozwa na Jaji ili kuchunguza sakata hilo undani.
Kakobe amfagilia Pinda
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospal Bible Fellowship, Zacharia Kakobe amemtetea Pinda kwa kumwelezea kuwa ni kiongozi shujaa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka 2013.
Pia, Kakobe amesema Waziri Pinda ana sifa zote za mtu anayefaa kuwa kiongozi, kwani ana moyo wa kishujaa licha ya kupata misukosuko akiwa kwenye nafasi yake ya uwaziri mkuu.
Akizungumza kwenye ibada ya Sikukuu ya Krismasi, Askofu Kakobe alisema: “Kati ya viongozi waliopo nchini mimi anaweza kusema kuwa Pinda ni kiongozi shujaa, kwani ametamka maneno mazito akiwa bungeni ambayo hadhani kama kuna kiongozi anaweza kuyatamka.“Neno la kwamba yupo tayari kuacha uongozi kwa sababu uongozi ni msalaba ni zito na kwamba ameonyesha kuwa yeye ni kiongozi makini asiyependa madaraka kama viongozi wengine.”
Askofu Kakobe alisisitiza kuwa anampongeza Pinda kwa moyo wake wa kishujaa na kuwataka viongozi wengine waige mfano wake.