Gari la waziri wa zamani wa Viwanda na Bishara, Dk Juma Ngasongwa likiwa limeharibika baada ya kupata ajali katika eneo la Picha ya Ndege, Kibaha juzi jioni. Picha ndogo, Dk Ngasongwa akiwa katika Hospitali Teule ya Tumbi alikopelekwa kwa matibabu baada ya kupata ajali hiyo. Picha zote na Chris Mfinanga.
Kibaha.
Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara, Dk Juma Ngasongwa (72) amenusurika kufa baada ya kupata ajali ya gari katika eneo la Picha ya Ndege, wilayani Kibaha, Pwani.
Ajali hiyo ilitokea saa 11 jioni ya juzi katika eneo hilo wakati Dk Ngasongwa akitokea Dodoma kwenda jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alithibitisha tukio hilo na kwamba Dk Ngasongwa alipata ajali hiyo akiwa na gari aina ya Toyota RAV 4 iliyokuwa ikiendeshwa na yeye mwenyewe.
Matei alisema katika tukio hilo, jamaa wa waziri huyo mstaafu, Salehe Ngayuna, aliumia na kupelekwa katika Hospitali Teule ya Tumbi kwa matibabu .
Alisema tukio hilo lilitokea baada ya gari hilo kugongana na lori aina ya Mitsubish, mali ya Tanesco.
Gari hilo lilikuwa linaendeshwa na Hussein Mnemwa (38) mkazi wa Dodoma.
Ofisa Habari wa Hospitali Teule ya Tumbi, Gerald Chami alithibitisha Dk Ngosongwa na mwenzake kufikishwa katika hospitali hiyo kwa matibabu.
“Ni kweli huyo waziri mstaafu aliletwa hapa Tumbi kama majeruhi wa ajali hiyo na alipatiwa matibabu na baadaye walimhamisha Muhimbili,” alisema.
Ofisa Uhusiano wa ya Muhimbili, Aminiel Eligaesha, alisema jana kuwa hakuna kumbukumbu zinazoonyesha kupokewa kwa waziri mstaafu huyo.
|
0 Comments