Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam.
Licha ya deni la taifa kuongezeka na kufikia Sh27 trilioni mwaka jana, Serikali imesema bado ina sifa za kuendelea kukopa kutokana na mapato ya ndani kuwa madogo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya alisema jambolinalozingatiwa na Serikali ni kuhakikisha fedha za mikopo zinatumika kwa shughuli za kukuza uchumi.
“Deni la taifa linajumuisha deni la Serikali kutoka vyanzo vyake vya mapato ya ndani na nje ya nchi pamoja na deni la nje ambalo Serikali imelidhamini kwa sekta binafsi,” alisema Mkuya.
Alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana, deni la taifa lilifikia Sh27 trilioni, kati ya kiwango hicho deni la nje ni Sh20.2 trilioni na ndani ni Sh6.8 1 trilioni, huku deni la nje la sekta binafsi likifika Sh3.5 trilioni.
“Tunaendelea kukopa na deni linaongezeka. Linaongezeka kwa mikopo inayochukuliwa na ile ambayo haijalipwa,” alisema.
Akitaja sababu za kuongezeka kwa deni hilo alisema: “Linaongezeka kwakuwa nchi bado inaendelea kukopa, kuendelea kuwepo kwa madeni ya nyuma kutokana na muda wake wa kuyalipa kutofika, kuongezeka kwa watu na shughuli za kiuchumi pamoja na kuwepo kwa madeni ambayo kwa mujibu wa mikataba yanatakiwa kusamehewa.”
Alisema kutokana na kuwepo kwa orodha ndefu ya nchi zinazokopa, hivi sasa Tanzania imejikita zaidi katika kukopa mikopo yenye masharti ya kibiashara ambayo ni tofauti na mikopo yenye masharti nafuu.
Hata hivyo, Mkuya alisema kila mwaka Serikali inafanya tathmini kama inaweza kuhimili deni kutokana na shughuli za kiuchumi ndani ya nchi. “Tathmini ya mwisho tumefanya Septemba mwaka jana, haifanywi na Serikali pekee, inahusisha pia Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) na Benki ya Dunia (WB),” alisema Mkuya.
Waziri huyo alivitaja viashiria vinavyoonyesha kuwa nchi ina uwezo wa kuhimili deni kuwa ni thamani ya deni la nje ikilinganishwa na uchumi wa nchi (GDP),”
“Deni la nje sasa hivi ni asilimia 25 ambayo ni sawa na asilimia 24.8 ya uchumi wa nchi. Lakini ukomo wa kukopa kwa kutumia kiashiria hiki ni asilimia 50 ya deni, hivyo bado tuna vigezo vya kukopa maana tupo katika asilimia 24.”
Alisema thamani ya leo la deni lote la taifa kwa uchumi wa nchi ni asilimia 40.5 na kwamba ukomo wake ni asilimia 74.
“Lakini hilo halitufanyi kukopa zaidi, ila kutokana na hali ya uchumi tutakopa katika vyanzo nafuu,” alinena.Alisema Serikali itaendelea kukopa na kuhakikisha kuwa mikopo inayochukua inaelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi, kama barabara, badari na reli.
Alisema kutokana na hali ya sasa ya uchumi, nchi imeanza kupokea misaada na kupata mikopo kutoka maeneo mbalimbali bila vikwazo vingi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Waziri alisema mikakati ya Serikali ni kupunguza deni hilo na kuimarisha upatikanaji wa mapato ya ndani.
Akizungumzia utekelezaji wa bajeti ya Serikali mwaka 2013, alisema, “Mapato yote kwa kipindi hicho yalifikia Sh7.1trilioni, kati ya mapato hayo mapato ya ndani yalikuwa Sh4.8trilioni wakati tulipanga kukusanya Sh5.7trilioni.”
Alisema katika kipindi hicho misaada na mikopo nafuu kutoka nje ya nch, ilikuwa Sh1trilioni, na kwamba Sh3.8trilioni zilizoahidiwa na nchi wahisani na mashirika ya kitaifa hadi sasa kiasi kilichopatikana ni asilimia 29 na kwamba Serikali ilikopa Sh507bilioni kutoka katika mapato ya ndani.
Kuhusu fedha kutoka hazina kutofika kwa wakati katika maeneo husika alisema, “Serikali tunakusanya mapato yetu kila mwezi na kupitia TRA tunapata Sh800bilioni kwa mwezi, fedha hizo hazitoshi sana na ikumbukwe kuwa hata fedha kutoka nje nazo huchelewa kutufikia.
Akizungumzia mashine za kutolea risiti za elektroniki (EfDs) ambazo Serikali ilisitisha matumizi yake baada ya kuibuka kwa sintofahamu kati ya Mamlaka ya Mapato (TRA) na wafanyabiashara wenye kipato cha kuanzia Sh14milioni hadi 40milioni alisema kuanzia Februari mosi mwaka huu mashine hizo zitaanza kutumika kama kawaida.
|
0 Comments