Aliyekuwa Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa enzi za uhai wake
Dar/Iringa. 
Serikali imesema itaweka wazi kilichomuua Dk William Mgimwa Jumapili, huku Katibu wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Martini Simangwa akisema marehemu Mgimwa atazikwa Jumatatu katika Kijiji cha Magunga kilichopo Kata ya Maboga mkoani Iringa.
Mwili wa Dk Mgimwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, unatarajiwa kuletwa nchini kesho ukitokea Pretoria, Afrika Kusini. Mgimwa alifariki dunia katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic iliyoko Pretoria alikokwenda kwa matibabu.
Wakati hayo yakielezwa, Serikali imeahidi kuweka wazi kilichomuua Dk Mgimwa wakati wa kumuaga marehemu Jumapili kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge,William Lukuvi, alisema kuwa kwa sasa ni mapema kueleza kilichomuua Dk Mgimwa.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Msemaji wa familia, Charles Nyato alisema mwili utawasili saa 7.00 mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na kupelekwa nyumbani kwake Mikocheni B, Mtaa wa Ruvu.
“Baada ya shughuli ya kuaga, siku hiyohiyo, mwili utasafirishwa kwa ndege kwenda kijijini, Magunga ukipitia Iringa mjini kutoa nafasi kwa wananchi kutoa heshima za mwisho kisha kwenda kijijini ambako mwili utalala kabla ya mazishi Jumatatu,” alisema Nyato.
Dk Shein atuma salamu
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za rambirambi Rais Jakaya Kikwete kutokana na kifo cha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
Katika salamu hizo, Dk Shein amemwelezea marehemu kwamba atakumbukwa kutokana na utumishi wake uliotukuka kwa Serikali na wananchi wa Tanzania.
“Tanzania imempoteza kiongozi shupavu, mpenda kazi, mzalendo na mtu mwenye busara na upendo kwa wenzake,” alisema.
Naye mtoto wa marehemu, Godfrey Mgimwa akizungumzia kifo cha baba yake alisema: “Kifo cha mzee ni pigo kubwa sana kwetu, inauma ila ndiyo mipango ya Mungu.
“Mzee alikuwa ni mtu anayependa haki na mpenda maendeleo, kiongozi bora na alikuwa akifanya kazi vizuri serikalini. Tumempoteza mtu muhimu sana,” alisema Godfrey kwa upole.“Mzee alikuwa na kawaida ya kwenda kuangalia hali ya afya yake na alikwenda AfrikaKusini kutokana na mazingira yake ya kazi, lakini kilichosababisha kifo bado hatukijui,” alisema Godfrey.
Akizungumza na gazeti hili kwenye Ofisi ya Mbunge iliyopo katika jengo la Siasa ni Kilimo la Halmashauri ya Iringa Vijijini, Simanagwa alisema mwili utakapowasili utasafirishwa hadi kijijini kwao Magunga, Kata ya Maboga katika Jimbo la Kalenga ambako ndiko alikozaliwa. Aidha aliwataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba
Wanasiasa walonga
Jirani wa muda mrefu wa Dk Mgimwa, Mbunge wa Namtumbo Mkoa wa Ruvuma (CCM), Vita Kawawa alisema kifo cha Dk Mgimwa ni pigo kubwa serikalini, jamii na jimboni kwa jumla.
“Nilimfahamu Dk Mgimwa hata kabla ya kuingia katika siasa, kipindi najenga vifaa nilikuwa naviacha kwake, inauma sana kumpoteza mtu muhimu, tutamkumbuka kwa mengi, tumempoteza kipindi ambapo taifa na wapiga kura wake walimtegemea. Hiyo yote ni mipango ya Mungu,” alisema Vita
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba alisema: “Chama na Taifa kimempoteza mtu makini na muhimu kutokana na kuwajibika ipasavyo, alifufua vyanzo vya mapato vilivyokuwa vimejificha.
“Ameondoka wakati tunamuhitaji...mara ya mwisho nakumbuka alisema ana matatizo ya figo sasa sijui ndio kilichosababisha kifo chake au la lakini tusubiri ripoti ya madaktari.”
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema: “Tangu nianze kufanya kazi sijawahi kukutana na kiongozi kama Dk Mgimwa. Alikuwa kiongozi na msikilizaji wa mawazo yanayotolewa na wengine, ametufundisha jinsi ya kuwa kiongozi.”
Aliongeza “Tumempoteza mtu muhimu kutokana na weledi wake katika kazi. Taifa, wapigakura wake na wananchi kwa ujumla tutamkumbuka kwa uongozi wake madhubuti.”
*Imeandikwa na; Ibrahim Yamola, Beatrice Moses (Dar) na Geofrey Nyang’oro, Iringa.