Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye |
Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema mwanachama yeyote anayetangaza nia ya kuwania nafasi ya urais kabla ya muda mwafaka kutangazwa, anapoteza sifa ya kuwa mgombea.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Dar es Salaam jana kwamba chama hicho kinaamini katika umoja na mshikamano na kwamba wanaotangaza nia ya kugombea urais kabla ya muda wamepoteza sifa kwa kuwa ni kama wanakigawa.
Juzi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alitangaza nia ‘kimtindo’ akisema anaanza rasmi safari aliyoiita ya matumani ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Lowassa ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, alitangaza hayo katika ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli.
Nape alisema wanaotangaza nia ya kuwania urais hivi sasa wanafahamu kwamba hawana sifa za kuwa wagombea wa nafasi hizo kwa sababu mbalimbali.
Alisema wanafahamu wazi kwamba vikao vya chama havitawapitisha kutokana na kutuhumiwa kwa rekodi zao pia ni mbaya.
“Suala hili liko wazi katika chama chetu, viongozi wenye sifa waliowahi kuongoza nchi hii hawakujitangaza mapema. Walisubiri na muda ulipofika wakatangaza nia ya kuwania,” alisema Nape.
Alisema kwa hao wanaojitangaza hivi sasa kabla muda, wanakigawa chama na kwamba vikao havitawapitisha labda wafanye hivyo kupitia vyama vingine.
“Labda wagombee urais kupitia vyama vingine lakini si CCM, chama hiki kina misingi na taratibu zake, wanachama wanashikamana hadi muda utakapofika,” alisema.
Alisema viongozi bora hawapatikani kwa kujiandaa wao wenyewe kuchukua nafasi hizo, bali kwa kuombwa na wanachama wenzao katika hatua mbalimbali zinazokubalika.
Urais CCM
Oktoba mwaka jana, Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Ali Shein alielezea kushangazwa na tabia ya baadhi ya wanachama wa CCM kutangaza nia ya kuwania nafasi za uongozi kwa uchaguzi wa 2015 ikiwamo nafasi ya urais wakati wahusika wa nyadhifa hizo bado hawajamaliza muda wao.Akifungua Mkutano wa Makatibu wa CCM wa Mikoa, Dk Shein aliwataka watu hao kusubiri hadi chama kitakapotoa mwongozo.
Katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwenye mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini, mwishoni mwa mwaka jana, alisema wanaotangaza nia mapema, wanajitengenezea mazingira magumu ndani ya chama.
Mbali na Lowassa, wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Ushirikiano waAfrika Mashariki, Samuel Sitta, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.
0 Comments