Pius Msekwa PICHA MAKTABA
Dar es Salaam. 
Wakati mjadala wa uteuzi wa mawaziri ukiendelea kupamba moto nchini, makada wakongwe wa CCM, Pius Msekwa na Peter Kisumo wamesema Rais Jakaya Kikwete ndiye mwenye mamlaka ya kuteua na habanwi na chama, wala mtu yeyote.
Wamesema chama kinaweza kumshauri Rais kuhusu uteuzi, lakini hakiwezi kumbana atekeleze uteuzi wa mawaziri kinaowataka.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Msekwa alisema mwenye mamlaka ya kufanya uteuzi wa mawaziri nchini ni Rais Jakaya Kikwete peke yake.
“Uteuzi wa mawaziri ni kazi ya Rais na katika hilo, hana ubia na mtu na ndiyo mfumo uliopo na unaeleweka na kila mtu na unatumiwa nakaribu nchi zote duniani,” alisema Msekwa ambaye ni Makamu wa Mwenyekiti mstaafu wa CCM Tanzania Bara.
Msekwa ambaye pia amewahi kuwa Spika wa Bunge alisema haoni tatizo la mfumo katika suala zima la utendaji kazi wa Serikali na kusisitiza kuwa Rais mpaka anafikia hatua ya kumteua mtu ni wazi kuwa anajua utendaji wake wa kazi.
Alipoulizwa kama haoni uteuzi wa Rais ni kinyume na maagizo ya Kamati Kuu ya chama hicho alisema: “Mawaziri waliitwa mbele ya kamati na kilichozungumzwa ndani ya kikao hicho mimi na wewe hatujui, pengine walijieleza vizuri na ikaonekana kuwa hawana tatizo na kuamua kuwarejesha bila kuwapa adhabu yoyote.”
Kisumo
Naye Kisumo ambaye ni Mdhamini wa CCM, alisema, Rais anaweza kutekeleza au kutokutekeleza uamuzi unaotolewa na chama chake.
Alisema: “Siyo kila linalosemwa na chama lazima Rais alitekeleze, hapana, kwani sijapata kuona mahali popote duniani Rais akatekeleza matakwa ya chama. Urais siyo chama.”
Aliongeza: “Kazi ya kubadili Serikali ni kazi ya Rais, kama chama kimeona kuna mawaziri mizigo hicho ni chama, lakini Rais anaweza kuteua yeyote anayeona anafaa.”
Alisema chama kinapotaka kusema au kutoa maoni yake juu ya jambo lolote hakiombi kibali kwa Rais kutokana na majukumu ya vyama vya siasa kuwa ni kuwatetea wananchi wake.
“Rais anapofanya mabadiliko yake ya Serikali, nje wananchi wanaweza kusema huyu anafaa au huyu hafai, lakini hiyo ni kazi ya Rais kuona kama wanafaa au hawafai.”Mawaziri waliohojiwa na CCM na kubakizwa katika Baraza la Mawaziri ni Dk Shukuru Kawambwa (Elimu), Christopher Chiza (Kilimo), Saada Mkuya (Fedha). Mkuya alihojiwa kwa niaba ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa ambaye kwa sasa ni marehemu.
Wengine ni Dk Abdallah Kigoda (Viwanda), Dk Mathayo David (Mifugo na Uvuvi) ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Kikwete,Celina Kombani (Utumishi wa Umma) na Hawa Ghasia (Tamisemi).
Madudu ya mawaziri hao yaliibuliwa na wananchi wakati wa ziara ya siku 26 iliyofanywa na baadhi ya watendaji wakuu wa CCM, mwishoni mwa mwaka jana katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe.
Kutokana na malalamiko hayo, Kamati Kuu ya CCM, iliwaita na kuwahoji mawaziri, kisha kumshauri Rais Kikwete mambo matatu; kuwafukuza, kuwahamisha wizara au kuwahimiza wafanye kazi.
Hata hivyo, katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri aliyoyafanya hivi karibuni, kujaza nafasi za mawaziri waliotenguliwa uteuzi wao kutokana na kashfa ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, Rais Kikwete aliwarejesha baadhi ya mawaziri waliotajwa kuwa ni mizigo.
Akizungumza na gazeti hili, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alisema: “Kitendo cha Rais Kikwete kuwabakiza mawaziri hao kwenye baraza lake ni sawa na kupuuza kilio cha wananchi na Kamati Kuu ya CCM.
Aliongeza: “Ndiyo maana nawashauri ndugu zangu Kinana na Nape waachie ngazi kwenye nafasi za uongozi wanazoshikilia ili kutoa nafasi kwa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama Taifa kuteua watu wengine atakaosikiliza maoni yao.
Mbunge huyo mwenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Bunge alisema: “Kimsingi yale si maoni yao binafsi, ni maoni yaliyoibuliwa na wananchi na kuongezewa nguvu na maoni ya wajumbe wa kikao cha Kamati Kuu ya CCM, hivyo Rais alipaswa kuyazingatia.”
Chadema wazungumza
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Taifa, John Heche amewataka Watanzania kukichukulia kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kulazimika kuwaacha kwenye baraza lake, mawaziri ambao walitajwa na chama chake kuwa ni mizigo, kama ishara ya chama hicho kufika mwisho.
Akizungumza katika mikutano ya hadhara ya M4C- Operesheni Pamoja Daima ya chama hicho inayoendeshwa nchi nzima, katika maeneo ya Mto wa Mbu, Karatu, Katesh, Mbulu na Babati jana, Heche amesema kuwa kitendo hicho kinapaswa kuchukuliwa na Watanzania kama ujumbe kwamba CCM kimechoka na kinapaswa kuondolewa madarakani.
Mwenyekiti huyo wa Bavicha ambaye yuko kwenye timu inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu alisema kuwa iwapo ndani ya CCM kungekuwa bado kuna watu wazuri wa kushika nafasi ya uwaziri, Rais Kikwete asingelazimika kuendelea kufanya kazi na watu ambao wametangazwa nchi nzima na chama hichohicho kinachounda Serikali kuwa hawafai.“Jamani katika hili la mawaziri mizigo tumshukuru Rais Kikwete kwa sababu ametuma ujumbe mkubwa kwa Watanzania kuwa ndani ya CCM hakuna tena watu wanaofaa. Ametusaidia kujua kuwa siyo kwamba tu kuna mizigo ndani ya chama chao,bali wamo watu ambao hawafai lakini ameamua kuwapatia nafasi kwenye uteuzi huu mpya.
“Kwa sababu kama kungelikuwa na watu wengine makini wanaofaa kuwa mawaziri au manaibu waziri, Rais Kikwete asingeweza kuthubutu kuendelea na watu ambao wametajwa kwa majina kuwa hawafai kuendelea kushika nafasi hizo. CCM wamefika mahali huwezi tena kupata mtu mwingine zaidi ya hawa mnaowaona. Ni dalili ya chama kilichochoka.
Mbali na kuhusisha suala hilo na kukosekana watu wengine ndani ya chama hicho, Heche pia alisema kuwa utamaduni wa kulindana unaendelea kukimaliza CCM kwa sababu kuna watu ambao hawawezi kuachwa nje ya uongozi kwa sababu wanapaswa kulindwa kwa nguvu zote.