Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (kulia) na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe wakitoka katika Ukumbi wa Bunge, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 
Dar es Salaam.
 Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC, imepanga kuzikutanisha kwa pamoja, Wizara za Fedha na Elimu wakati ikipokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayohusu matumizi ya fedha za marejesho ya rada jinsi zilivyotumiwa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deo Filikunjombe alisema kuwa wanatarajia kupokea taarifa hiyo kesho na watatumia fursa hiyo kujihakikishia kama matumizi hayo yalikuwapo au kama kulikuwa na ulaghai wa aina yoyote.
“Kwa sasa ni mapema kuanza kufikiri kwamba fedha hazikutumika inavyotakiwa, lakini kama kuna ujanja wowote ulifanyika tutabaini tu alisema na kuongeza:
“Ndiyo sababu katika kikao hiki tunakutana wote; CAG, Wizara ya Fedha na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kama kuna maswali basi kuwe na majibu yake papo hapo,” alisema Filikunjombe.
Alisema leo watapokea taarifa ya ukaguzi maalumu kuhusu mbolea ya ruzuku, pia shughuli nyingine ambazo kamati inatarajia kuzifanya katika kipindi cha wiki mbili zijazo ni pamoja na kutembelea bandari na kukagua mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe wilayani Ludewa.
Awali mwaka jana aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene, aliliambia Bunge kwamba fedha za rada zilizorejeshwa Sh72.3 bilioni ziliingizwa katika bajeti ya serikali kwa mwaka 2012/13.
Mbene alisema kwamba fedha hizo ni marejesho kwa Serikali ya Muungano kutokana na udanganyifu uliofanywa na Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza wakati wa kuiuzia Serikali ya Tanzania rada ya kuongozea vyombo vya usafiri angani.
Fedha zilizorudishwa na kampuni hiyo baada ya Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza kubaini kuwa, baadhi ya maofisa wa Serikali ya Tanzania na mawakala wa ununuzi kupandisha bei baada ya kushawishiwa na kampuni hiyo.
Novemba mwaka jana Serikali ilianza kusambaza vitabu milioni 19.4 kwa shule za msingi nchini, ambavyo ilielezwa kuwa vimenunuliwa kwa chenji ya rada na asilimia 75 ya fedha hizo zimetumika kununulia vitabu hivyo na asilimia 25 zitatumika kununulia madawati.