Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha,Stella Mugasha (kulia) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Mawakili wa kujitegemea mkoa wa Arusha, Modest Akida walipohudhuria maadhimisho ya Siku ya Sheria iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu jijini Arusha jana. Picha na Filbert Rweyemamu 
Dar/Mikoani. 
Rais Jakaya Kikwete amewataka wadau wa haki na sheria na vyombo vyote kushirikiana pamoja katika utendaji kazi, ili kuwawezesha walengwa kupata haki zao kwa wakati.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika viwanja vya Mahakama Kuu jana, Rais Kikwete alisema ni ukweli usiopingika ili haki itolewe kwa wakati inahitaji ushiriki wa wadau wote wanaosimamia haki na sheria.
“Polisi, wanasheria, mahakimu na majaji na Serikali, wote kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake ili kufanikisha hili la kupatikana haki kwa wakati,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mahakama haipelelezi kesi, haikamati mshtakiwa, haiendeshi mashtaka na wala haimtetei mtuhumiwa au mlalamikaji… utaona hapa kila idara inalo jukumu la kutimiza wajibu wake,” alisema.
Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande alisema maudhui ya Siku ya Sheria yanaendana sambamba na Dira ya Mahakama ya kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati, na ile ya Wizara ya Katiba na Sheria ya Kutoa Haki kwa Wote kwa wakati.
Jaji Othman alisema mfumo bora wa utoaji haki ni ule wenye fursa ya haki na unatenda haki sawa kwa wakati, kwa gharama nafuu, ulio wazi na unaoaminika na unaoendeshwa na maofisa na watendaji waadilifu.
Kupanua mtandao
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Stella Mugasha alisema wanakusudia kuanzisha vikao vya makosa ya jinai wilayani Karatu, ili koboresha huduma wilaya za Ngorongoro, Karatu na Mbulu.
Kufanya hivyo, alisema kutaondoa kero ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.
Washauri ukomo wa upelelezi
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kagera, Gad Mjemas alishauri kufanyika marekebisho ya sheria zinazokwamisha upatikanaji haki kwa wakati.
Alisema sheria haijaweka ukomo kwa baadhi ya washtakiwa kukaa mahabusu muda mrefu.Viongozi wakemewa
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Noel Chocha alisema kuwa tamaa ya baadhi ya viongozi kujiingiza kila eneo ambalo hata halimhusu, ni kiini na sababu ya kuwapo kwa mvurugano wa utendaji.
Alisema licha ya Katiba ya nchi kuelekeza misingi ya mgawanyo wa madaraka, miongoni wa watumishi wapo wanaokiuka ama kwa kutojua au makusudi.
Kesi zisikilizwe kwa wakati
Waziri Mkuu Msataafu, Fredrick Sumaye amezitaka mahakama nchini kufuata na kusimamia maelekezo yaliyotolewa na jaji mkuu na majaji wafawidhi kuhakikisha wanatekeleza muda wa kesi mahakamani usizidi miezi 18.
Akizungumza mjini Kibaha, Sumaye alibainisha iwapo maagizo na uamuzi huo utatekelezwa utajenga imani kwa wananchi.
Habari hii imeandaliwa na Joyce Mmasi, Dar esSalaam; Filbert Rweyemamu, Arusha; Phinias Bashaya,Bukoba; Godfrey Kahango, Mbeya na Julieth Ngarabali, Kibaha.