Balozi wa Uingereza nchini, Diana Melrose (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi wa Wanyama Pori, Prof Alexander Songorwa (katikati) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi baada kuhudhuria mkutano wa wizara hiyo na mabalozi wa nchi mbalimbali nchini uliofanyika jana. 
Dar es Salaam. 
Jumuiya ya Kimataifa imeungana na Tanzania katika vita ya dhidi ya ujangili na vita hiyo itaongozwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP).
Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ikisema awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza Ujangili i itaanza muda wakati wowote kuanzia sasa.
Akizungumza na mabalozi wa nchi mbalimbali nchini katika kikao cha kujadili njia shirikishi ambazo jumuiya hiyo itashirikiana na Tanzania katika vita hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema UNDP itakusanya fedha na misada mbalimbali kutoka nchi wahisani ili kufanikisha mpango huo. Operesheni hiyo ilisitishwa kwa muda baada ya kukumbwa na kasoro kadhaa ikiwa ni pamoja na kuuwa kwa watu na mifugo.
Hali kadhalika, uharibifu wa mali, hatua iliyomlazimisha Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wanne ambao wizara zao zilitajwa kushindwa kusimamia operesheni hiyo.
“Nchi mbalimbali zimekubali kuisaidia Tanzania katika mikakati yake ya muda mrefu na mfupi ya kupambana na ujangili. Baadhi ya nchi hizo ni Uingereza, Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Hispania, Japan na China. Pia kuna Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Umoja wa Mataifa (UN),” alisema.
Alisema nchi hizo zimekubali kuisaidia Tanzania kutokana na ombi la Rais Kikwete ambaye aliziomba kusaidia kwa vitendo vita hiyo.
“UNDP ndiyo wataiunganisha Serikali na mashirika ya maendeleo katika kukusanya fedha na misaada mbalimbali ambayo tutakubaliana kwa pamoja itumikeje katika mikakati ya Serikali ya muda mfupi na mrefu” alisema Nyalandu. Kwa mujibu wa waziri kwa sasa kuna uhaba wa askari 3,767 wa wanyamapori na kwamba askari waliopo ni 1,088.
Alisema Serikali itashirikiana na nchi hizo kuhakikisha kuwa inapambana na wanaoua wanyamapori, utoroshaji wa rasilimali kupitia viwanja vya ndege, bandari na maeneo mengine.
“Wenzetu pia watatusaidia hadi katika nchi ambazo meno ya tembo na faru hupelekwa kwa ajili ya kuuzwa. Pia tutawatumia zaidi Polisi wa Kimataifa (Interpol).”
Malalamiko askari
Akizungumza kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli kwamba zaidi ya askari 2,000 waliounda kikosi maalum kwa ajili ya operesheni hiyo, hawajalipwa posho zao, Nyalandu alisema watalipwa kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya operesheni hiyo.
“Askari wote walioshiriki katika operesheni hii watalipwa kabla ya kuanza kwa awamu ya pili. Hili ni zoezi endelevu, lilisitishwa baada ya kuibuka kwa kasoro kadhaa. Askari poli, askari wanyamapori na JWTZ watalipwa,” alisema Kauli za mabalozi
Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose alisema nchi yake itaisadia Tanzania katika vita dhidi ya ujangili.
Dk Filberto Sebregondi ambaye ni Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), aliishauri Serikali kushirikiana na wadau katika vita hiyo.