Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akitangaza kuwaondoa wakurugenzi mbalimbali wa wizara yake mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amewaondoa katika nyadhifa zao, Wakurugenzi mbalimbali kwa sababu zilizoelezwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Hatua ya Nyalandu imekuja ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Bunge la Desemba 22, 2013 lililotaka Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kuwajibishwa kutokana na tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa haki za binadamu katika Operesheni Tokomeza.
Nyalandu alisema: “Namwondoa Prof Alexander Songorwa (Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori) na kumteua Paul Sarakikya kukaimu nafasi hiyo.”
Alisema pia kuwa amemwondoa Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Profesa Jafari Kidegesho kwenye nafasi hiyo na Dk Charles Mulokozi ameteuliwa kushika wadhifa huo.
Mwingine aliyeteuliwa ni Julius Kibebe kuwa Mkurugenzi Msaidizi Uzuiaji-Ujangili, nafasi iliyoachwa wazi na Sarakikya wakati Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu, Nebbo Mwina anabaki kwenye nafasi yake.
Nyalandu alisema Herman Keiraryo anaendelea kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji wa Wanyamapori na kwamba waliotangazwa kuondolewa kwenye nyadhifa, kazi zao mbadala zitatangazwa baadaye.
Waziri Nyarandu alitoa siku 30 kwa Wakurugenzi Wakuu wa kila Idara, Shirika na Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, kutengeneza viashiria vya utendaji kazi (Key Performance Indicators) na kuvikabidhi kwake.
Alisema hatua hiyo itafanikisha kufikiwa malengo ya wizara hiyo, kwani uwajibikaji na ufanisi wa kazi za kila siku utapimwa katika hali ya uwazi ili mikakati ya wizara itekelezwe katika mifumo inayopimika na hatimaye kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Waziri huyo aliagiza kila mtumishi akiwamo yeye mwenyewe, kutekeleza majukumu yaliyopangwa kwa kuzingatia kanuni za mwenendo (code of conduct), zitakazopendekezwa na kupitishwa na Baraza la Wafanyakazi la wizara hiyo.
|
0 Comments