Mwenyekiti Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT), Dk Reginald Mengi {katikati}
Dar es Salaam. 
Mwenyekiti Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT), Dk Reginald Mengi amesema vyombo vya habari vinapaswa kuwataja kwa majina watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa katika taasisi za umma, badala ya kutoa tuhuma za jumla.
Dk Mengi alisema tuhuma za jumla kwamba taasisi fulani ya umma inajihusisha na rushwa, zinawaumiza watumishi waadilifu ambao ni sehemu ya taasisi hizo.
“Mnapotoa tuhuma za jumla kwamba taasisi fulani inanuka rushwa, mnawaumiza wale watumishi waadilifu, tuhuma za aina hiyo zinawaficha wale waovu wanaohusika,” alisema Dk Mengi kwenye hafla aliyoiandaa kuwapongeza wahariri walioshinda kesi ya uchochezi iliyokuwa ikiwakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Waliokuwa wakikabiliwa na kesi hiyo ni aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti laTanzania Daima, Absalom Kibanda na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Theophil Makunga.
Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) hivi sasa ni Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd wakati Makunga ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya TEF, hivi sasa ni Meneja Uendelezaji Biashara wa MCL.
Katika hafla hiyo, Dk Mengi aliwataka waandishi wa habari kufanya uchunguzi wa kina wanapoandika habari kuhusu rushwa na kuwataja wahusika kwa majina, ili kuepusha tuhuma za jumla kwa taasisi.
“Waandishi wa habari msiwe waoga, kama kweli mtu anakula rushwa na ushahidi upo, hata akiandikwa nawahakikishia kwamba hawezi kwenda mahakamani kushtaki. Lakini, mkisema mfano kwamba polisi kunanuka rushwa au mahakama kunanuka rushwa, unampa ahueni mtuhumiwa halisi na kuwaumiza wengine ambao ni waadilifu,” alisema Dk Mengi.