Dar es Salaam. Wale wanaopenda kuvaa bidhaa za asili wapo hatarini kuburutwa kwenye vyombo vya sheria baada ya Serikali kudhamiria kwa dhati kuzuia biashara ya meno ya tembo hata katika bidhaa za vidani, mikufu, bangili au mikanda yenye nakshi ya meno ya tembo yaliyonunuliwa kihalali.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu katika Mkutano wa Kimataifa wa kujadili namna ya kukabiliana na ujangili amesema, Serikali imedhamiria kwa dhati kuzuia biashara ya meno ya tembo iwe katika bidhaa halali au katika soko haramu.
Nyalandu alisema, agizo la Rais lililotolewa katika mkutano huo ni kusitisha kabisa biashara ya meno ya tembo hata kwa bidhaa kama za mikufu, vidani, hereni na mikanda ya kiunoni.
“Kwa kifupi tumeamua kuwa watu wajiepushe na bidhaa zozote zenye meno ya tembo, ziwe kihalali au namna nyingine huenda wakaingia matatani,” alisema Waziri Nyalandu.
Nyalandu alisema nia ni kuondoa kabisa meno ya tembo katika mnyororo wa kiuchumi na kibiashara.
Katika mkutano huo, Rais Jakaya Kikwete pia aliamuru kuwa, hata biashara ya meno ya tembo yaliyohifadhiwa katika ghala ambayo yangeweza kuuzwa kihalali na Serikali, sasa hayatawekwa tena kwenye mnyororo wa biashara.
Nyalandu alisema licha ya kuwa mataifa mengine yanaishutumu Tanzania kuwa haifanyi jitihada za kutokomeza ujangili, Serikali kupitia wizara yake, imefanikiwa kuwakamata majangili wenye vyeo na utaifa mbalimbali 320 katika kipindi cha miaka mitatu, 2011 hadi 2013.
Alisema miongoni mwao wengi ni Watanzania, raia wa Bara la Asia na Ulaya.
“Waliponihoji kuhusu kutaja majina ya majangili niliwaambia kuwa, yapo majina ya majangili wengi hata raia wenu wa hapa Ulaya ninayo majina yao,” alisema.
Nyalandu alizungumzia kuhusu majangili wenye vyeo nchini na kusema kuwa, Serikali ilishawahi kuwakamata hata viongozi wa Serikali wa ngazi za wilaya waliokuwa wakifanya ujangili na wamechukuliwa hatua.
Katika kupambana na ujangili, Waziri Nyalandu alisema hivi sasa Serikali imeazimia kudhibiti mtandao wa ujangili unaojipanga kufanya ujangili badala ya kuwakamata majangili wenye meno tayari.
“Tunachokitaka ni kuwakamata wale ambao wako katika harakati au mipango ya kufanya ujangili na sio kukamata watu ambao tayari wameshaua tembo,” alisema.Aliongeza kuwa kwa sasa vita ya ujangili itaendeshwa kwa kuongeza wigo wa kiintelijensia sambamba na kuwatumia raia wema kutaja mtandao wa ujangili.
|
0 Comments