“Matrekta hayo yatakuwa yakitolewa kwa mkopo na tutachagua mojawapo ya benki, ambapo watu wataomba mikopo na kuirejesha hukohuko benki.”PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam.
Kampuni ya Equator Suma JKT yenye ubia na Shirika la Uzalishaji mali la Jeshi la Kujenga Taifa, imesaini mkataba na kampuni ya Farmer kutoka nchini Poland utakaowezesha uzalishaji wa matrekta Tanzania.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Equator Suma JKT, Ramesh Patel alisema kuwa mradi huo unagharimu Dola 70 milioni (Sh112 bilioni) ambazo ni mkopo kutoka Poland.
“Kwa muda mrefu, Serikali imekuwa ikizungumzia maendeleo ya kilimo, sisi tumeliona hilo na tulikuwa na mazungumzo na Kampuni ya Farm ya Poland,” alisema Patel na kuongeza:
“Leo ni siku ya kihistoria, kwani tunatia saini mkataba huu kuonyesha kuwa tuko tayari kuzalisha matrekta hapa nchini na yataitwa kwa jina la Kitanzania.”
Alisema mradi huo utaanza kwa kuzalisha matrekta machache ambayo yatafanyiwa majaribio na Kituo cha zana za kilimo na teknolojia vijijini (Carmatec) cha Arusha ili kuyathibitisha kwa ubora wa kimataifa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa kampuni ya Farm kutoka Poland, Robert Parcia alisema kuwa wameichagua Kampuni ya Equator Suma JKT kutokana na ufanisi wake katika kilimo.
“Leo ni siku ya furaha kwetu kwani tumeingia kwenye hatua mpya. Tunatarajia kwanza kuunganisha matrekta 1,200 kwa mwaka na hiyo itaanza mwaka 2017. Yatakuwa matrekta ya kiwango cha juu na ubora wake utakuwa ni kama wa Ulaya,” alisema Parcia na kuongeza: “Tunashukuru kwa kuwa Serikali ya Poland imetupa msaada wa kifedha ndiyo maana tunapata uhakika wa mafanikio.”
Naye Mkurugenzi wa Equator Suma JKT, Robert Ndege alisema matrekta hayo hayatakuwa kwa soko la Tanzania tu, bali kwa Afrika nzima.
“Wameichagua Tanzania kwa sababu ya uzuri wa eneo la kibiashara. Tutazalisha matrekta, siyo kwa soko la Tanzania tu, bali kwa Afrika nzima. Lengo letu ni kuhamisha teknolojia hiyo, ikiwezekana asilimia 70 itengenezwe kwao na sisi asilimia 30,” alisema.
“Matrekta hayo yatakuwa yakitolewa kwa mkopo na tutachagua mojawapo ya benki, ambapo watu wataomba mikopo na kuirejesha hukohuko benki.”
Alisema kuwa mradi huo utakuwa endelevu na hautaishia tu kuzalisha matrekta bali utakuwa pia ukizalisha magari aina nyingine.
“Kiwanda hiki kimeanzishwa kwa ajili ya uzalishaji wa matrekta, lakini tutazalisha na magari mengine. Tunategemea kuendelea na uzalishaji kwa zaidi ya miaka 200 ijayo,” alisema Ndege na kuongeza:“Hiki kiwanda kitakuwa cha Watanzania licha ya kusaidiwa na Poland. Tutakachokifanya ni kuwafundisha Watanzania utaalamu huu ili tuzalishe zaidi. Hata Poland wakiondoka, bado tutajitegemea.”
|
0 Comments