Makamu wa Rais wa zamani wa Sudan Kusini Riek Machar analaumiwa kwa kupanga njama yamapinduzi
Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan Kusini na waasi wanaoongozwa na aliyekuwa naibu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar yanatarajiwa kuanza tena leo mjiniAddis Ababa Ethiopia.Mazungumzo hayo yaliahirishwa mapema mwezi huu baada ya mazungumzo ya hapo awali kukwama.Aidha, pande zote mbili zimetuhumiwa kwa kukiuka mkataba wa kusitisha mapigano uliotiwa saini mwezi Januari.
Mnamo siku ya Jumatano, mataifa ya magharbi yanayohusika na mgogoro huu wa Sudan Kusini katika kuutafutia suluhu la kudumu, walitishia kuwawekea vikwazo wahusika wakuu kwenye mgogoro huo ikiwa hawatausuluhisha.
Mazungumzo ya kuzipatanisha pande hizo hayajapiga hatua kwa wiki mbili zilizopita huku wahusika wakilaumiana.Nao mkataba wa amani uliotiwa saini kusitisha vita pia haujafanikiwa katika kumaliza mgogoro huo.
Baadhi ya wanadiplomasia kutoka nchi za magharibi, wamehoji ikiwa viongozi wamejitolea kikweli kutafuta muafaka huku kila mhusika akimlaumu mwenzake kwa kizungumkuti kilichoko.
Mazungumzo hayo yanaanza tena baada ya wiki mbili ya kusitishwa kwake, ingawa wajumbe wamesema haijulikani ikiwa pande hizo mbili zitakuwepo.
Maswala makuu yanayoyumbisha mazungumzo hayo, ni matakwa ya waasi wa Sudan Kusni kwamba wafungwa wanne wa kisiasa ambao bado wanazuiliwa, sharti waachiwe huru.
Wanne hao walilaumiwa kwa kupanga njama ya mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir wakiongozwa na aliyekuwa makamu wa Rais Riek Machar