Wauguzi wa hospital ya Temeke ya jijini Dar es Salaam wakifurahia msaada wa mashine ya joto inayosaidia watoto wachanga waliozaliwa kabla ya muda wake (Njiti). Picha na maktaba
Dar es Salaam.
Wakati Serikali ikihangaika kutafuta ‘mwarobaini’ wa vifo vya wanawake wajawazito wanapojifungua, imebainika kuwa kuna idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wake (njiti), ambao hufariki dunia kila siku katika hospitali mbalimbali nchini kutokana na kukosa huduma.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika hospitali mbalimbali za Serikali jijini Dar es Salaam na mikoani, umebaini kuwa baadhi ya watoto hao hupoteza maisha kutokana na kukosekana kwa mashine maalumu za kuwahifadhia zijulikanazo kama ‘Incubator’.
Kwa mujibu wa Shirika la Mama Ye! Linalojihusisha na afya ya mama na mtoto, linasema kuwa kila mwaka watoto 210,000 huzaliwa kabla ya kutimiza muda wake, ambapo kati yao watoto 13,900 hufariki dunia, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya 12 kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto njiti duniani.
“Watoto wanaozaliwa mapema wana uwezekano wa mara sita hadi 26 kufariki dunia katika wiki nne za kwanza, ukilinganisha na watoto wanaozaliwa katika muda wake,” inasema sehemu ya ripoti ya Mama Ye!
Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto na wanawake katika shirika hilo, Dk Moke Magoma anasema wanaume pia wanamchango mkubwa katika kuwaokoa watoto njiti, kwani wanaweza kuwasaidia wake zao kuwaweka watoto vifuani ili wapate joto.
Alitoa mfano, daktari huyo anasema kuwa mwaka 2012 mwanamume mmoja mjini Zanzibar, aliokoa maisha ya mtoto wake kwa kumweka kifuani na kisha kumfunga kwa nguo baada ya mke wake kujifungua watoto mapacha njiti.
Hata hivyo, ripoti ya mwaka 2014 iliyotolewa na Shirika la Save the Children, watoto 36, 528 hupoteza maisha kila mwaka siku moja kabla ya kuzaliwa.
Watoto njiti milioni 15.1 huzaliwa kila mwaka duniani kote, idadi ambayo inamaanisha kuwa mtoto mmoja kati ya 10 huzaliwa njiti.
“Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa watoto wa kiume wana asilimia 14 ya kuzaliwa njiti ikilinganishwa na wa kike, hata hivyo, watoto wa kike wanauwezekano mkubwa wa kufariki dunia kuliko wa kike kutokana na lishe duni,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inasema kuwa mtoto njiti ambaye hufanikiwa kuishi husumbuliwa na matatizo ya muda mrefu kama uono hafifu, kutokusikia ipasavyo na maradhi sugu ya mapafu.
Katika Hospitali ya Amana, Wilaya ya Ilala, zaidi ya watoto njiti 60 huzaliwa kwa mwezi (sawa na asilimia 13 ya watoto wote), ambapo Februari mwaka huu jumla ya watoto 467 walizaliwa wakiwa na matatizo mbalimbali ya kiafya.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni hospitalini hapo, Daktari Bingwa wa watoto, Dk Mtagi Kibatala anasema kuwa zaidi ya wajawazito 70 hujifungua kila siku katika hospitali hiyo, idadi ambayo ni sawa na watoto 2,100 kwa mwezi na 25,200 kwa mwaka.Akizungumzia namna wanavyookoa maisha ya watoto wanaozaliwa njiti, anasema kwamba wale wanaozaliwa wakiwa na uzito chini ya kilo moja ndiyo walio katika hatari zaidi ya kufariki dunia, hivyo huwekwa kwenye mashine ya ‘Incubator’ kwa muda utakaopendekezwa na daktari kulingana na hali ya kiafya ya mtoto.
Hata hivyo, kutokana na uhaba wa mashine hizo hospitalini hapo, kwani zipo mbili tu, wahudumu hulazimika kuwapeleka watoto hao katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambayo ina wodi maalumu la kuhudumia watoto wa aina hiyo.
“Watoto wanaozaliwa chini ya kilo moja siyo wengi, watoto wengi wanaozaliwa ‘premature’ (njiti) wanakuwa na uzito kati ya kilo moja hadi kilo moja na nusu,” anasema Dk Mtagi.
Daktari Kiongozi wa hospitali hiyo, Dk Andrew Method anasema hospitali hiyo inahitaji mashine za 10 za ‘Incubator’, kwa sababu kuna wakati ambapo watoto zaidi ya 60 huzaliwa siku moja, kati yao 10 hadi 15 huhitaji msaada wa mashine hizo.
Anasema kuwa ukosefu wa mashine za kutosha unailazimu hospitali kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi, ambao watawahudumia watoto kwa karibu zaidi kwa kufuatilia maendeleo ya afya, ikiwa ni pamoja na kubaini kasoro yoyote inayoweza kujitokeza.
“Inapotokea mtoto anahitaji msaada wa haraka wa mashine halafu wakati huo kwenye mashine kuna mtoto mwingine, huwezi kusema umwondoe aliye ndani ili umweke mwingine,” anasema Dk Andrew.
Naye, Ofisa Muuguzi wa wodi ya watoto katika hospitali hiyo, Dk Mikali Msangi anasema kuwa watoto wengi wanaozaliwa hospitalini hapo hufariki dunia kutokana na kukosa hewa ya oksijeni kwenye ubongo (birthasphixia), kinyume na ripoti ya Shirika la Afya Dunia (WHO) inayoonyesha kuwa watoto wengi hufariki duniani kwa sababu ya kuzaliwa njiti.
Hata hivyo, Mganga Mfawidhi wa hospitai hiyo, Dk Meshack Shimwela anasema kuwa mashine za ‘Incubator’ zimepitwa na wakati kwa kuwa siku hizi inatumika njia mbadala ambayo humwezesha mama mzazi kumweka mtoto kifuani, ili pate joto (Kangaroo mother care).
Anasema hospitali nyingi hivi sasa zinatafuta nafasi ya kutosha ili ziweze kuongeza vitanda vya kumwezesha mama kukaa na mtoto wake muda wote, badala ya kumweka mtoto kwenye mashine.
Pia, anaongeza kuwa hata mashine za ‘incubator’ zilizopo hospitalini hapo zimepoteza kazi kwani kama kuna mtu anazihitaji kuzinunua anaweza kuuziwa. “Siku hizi hatuzitaki hizo mashine, hata kama kuna mtu unamfahamu anazitaka, mlete aje azinunue,” anasema Dk Meshack.
Akitaja matatizo ya mashine hizo, Dk Meshack anasema kuwa wakati mwingine joto huzidi kiwango kinachotakiwa na hivyo kuhitaji mtu wa kuirekebisha mara kwa mara. Pia mashine hizo hushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na ukosefu wa umeme wa uhakika.
“’Incubator’ inafaa kama mama amekufa amemwacha mtoto, ndiyo tunaweza kumweka mtoto kwenye mashine,” anaeleza na kuongeza:“Kwa njia ya Kangaroo tunahitaji nafasi ya kutosha na maji, kwa sababu mama anatakiwa awe msafi wakati wote.”
Anasema Hospitali ya Amana ina vitanda sita wakati Muhimbili vipo 40 vinavyotoa huduma ya Kangaroo na kwamba utaratibu huo unapendwa na wazazi kwa sababu unawawezesha kuwa karibu na watoto wao muda wote.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Marina Njelekela anasema kuwa matibabu kwa njia ya Kangaroo yanafaa zaidi kuliko matumizi ya ‘Incubator’, kwa sababu yana gharama ndogo, mama anakuwa karibu na mtoto pia joto linakuwa katika kiwango kinachotakiwa wakati wote.
“Ni njia nzuri lakini mzazi haruhusiwi kuifanya pekee yake nyumbani, kwa sababu anaweza kumwacha mtoto akapatwa na baridi akafariki dunia,” alisema Dk Njelekela.
Anapoulizwa iwapo matumizi ya ‘Incubator’ yamepunguza vifo vya watoto njiti nchini anasema: “Sina data (takwimu) sahihi, labda ongea na daktari ambaye anahusika na Kangaroo,” kisha anatoa namba ya simu ya daktari wa watoto, Dk Mary Charles ili atolee ufafanuzi suala hilo.
Hata hivyo, namba hiyo ilipigwa kwa siku tatu bila mafanikio, kwani kila mara ilikuwa ikisema kuwa namba hiyo haipo, hata alipoulizwa Dk Njelekela alimtaka mwandishi aendelee kupiga badaye itakubali.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Sophinias Ngonyani anasema kuwa zipo hospitali mbili tu jijini Dar es Salaam ambazo zina wodi maalumu za kuwahudumia watoto njiti.
Hospitali hizo za Mwananyamala na Muhimbili, zina vyumba maalumu vyenye huduma zote muhimu kwa ajili ya watoto hao, hata hivyo, wakati mwingine huzidiwa kutokana na idadi kubwa ya watoto wanaolazwa kwa siku moja.
Dk Ngonyani anasema kuwa Hospitali ya Mwananyamala ina uwezo wa kulaza watoto njiti 20 kwa wakati mmoja, lakini hupokea zaidi ya watoto 80.
Hospital ya Mkoa wa Ruvuma
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma Dk Daniel Malekela, amesema tatizo la wajawazito kujifungua watoto njiti limetokana na kumeza dawa bila kupata ushauri wa daktari au wataalamu wa afya, ambapo sababu nyingine magonjwa yanayotokana na ujauzito wenyewe na mji wa mimba na uchungu kuanza mapema.
Dk Malekela amefafanua kuwa kwa sasa hospitali hiyo ina mashine mbili za kutunza watoto njiti ingawa hawazitumii na wanatumia njia ya kangaroo ambapo mama akishajifungua ulazimika kukaa kwenye chumba chenye joto jingi na kumbeba mwanaye ngozi kwa ngozi ili kuweza kumsaidia apate joto na kuongezeka kilo kwa muda mfupi ambapo njia hiyo imesaidia zaidi kuokoa watoto wengi na vifo tofauti na kutumia mashine.
Amesema bado hakuna takwimu kamili za watoto wanaozaliwa kabla ya siku katika hospitali hiyo, ingawa tatizo hilo lipo na linachangiwa na sababu nyingi ikiwemo mama mjamzito kujifungua kabla ya wakati ingawa utafiti bado haujaonyesha sababu maalumu ya tatizo hilo.
Dk Malekela amewashauri wanawake wajawazito kuacha kumeza dawa bila kupata ushauri wa kitaalamu, ikiwa ni pamoja na kuacha tabia ya kuzembea kwenda kliniki kwani wanapoanza kliniki wakiwa na ujauzito wa wiki 16 wanasaidiwa na wataalamu kugundua matatizo mbalimbali waliyonayo baada ya kufanyiwa uchunguzi hivyo kuwasaidia kujifungua salama.
Huduma ya kuwatunza watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, imesaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga hospitalini hapo.
Huduma hiyo inayotambulika kama kangaroo, yaani ngozi kwa ngozi imekuwa mkombozi kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwa Mkoa wa Kilimanjaro, kwa kuwa ni hospitali pekee inayotoa huduma hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, mtaalamu wa magonjwa ya watoto kutoka KCMC, Dk Aisa Shayo alisema hospitali hiyo haina ‘Incubator’ lakini kutokana na huduma ya kangaroo kwao imekuwa mkombozi.
“Sisi hatuna ‘Incubator’ lakini tumekuwa tukiwafundisha kinamama jinsi ya kuwatunza watoto kwa kutumia njia ya kangaroo, ambayo mama humlaza mtoto juu ya kifua chake na kukutanisha ngozi zao huku mtoto akiwa amevaa nepi, kofia na soksi na mama atapaswa kumfunika na nguo nyingi kumwongezea joto.”
Akizungumzia tatizo la ongezeko la watoto njiti, Dk Shayo alisema kwa sasa uelewa wa wanajamii juu ya watoto njiti ni mkubwa na hivyo wengi wao kuwapeleka hospitali mapema pindi wanapozaliwa na kuona ni jambo la kawaida tofauti na miaka ya nyuma ambapo watoto hao walionekana ni tatizo kwenye familia.
Alisema hospitali hiyo inauwezo wa kuwatunza watoto 17 kwa wakati mmoja, ambao wanaozaliwa njiti na kwamba kati yao 10 huhifadhiwa kwenye vitanda maalumu vyenye joto na saba huishi na wazazi wao kwa mfumo wa kangaroo.
Dk Shayo alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni uhaba wa vitanda, hita ya umeme ambazo hufungwa vitandani ili kukiwezesha kitanda kuwa na joto na kinamama kutokukubali kuwaweka watoto kifuani wakiona ni usumbufu.
Alisema ili kukabiliana na ongezeko la watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ni vyema kinamama kwenda kliniki mapema, pindi anapopata ujauzito ili kupata ushauri wa kidaktari pamoja na kula lishe bora na kamili ili kumwezesha mtoto kukua.
Waziri
Gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, lakini simu yake ilipokelewa na katibu wake ambaye alisema kuwa waziri yupo kwenye kikao na kwamba apigiwe simu Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Kinga, Dk Neema Rusibamayilla, ambaye hata hivyo alikuwa nje ya nchi.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen Kebwe anasema hakuna ongezeko kubwa la idadi ya watoto njiti wanaofariki dunia, bali hali hiyo inaweza kuwa imesababishwa na ongezeko la asilimia 2.8 la Watanzania kwa mwaka.
Dk Kebwe anasema siyo sahihi kusema kuwa idadi ya vifo vya watoto nchini imeongezeka, kwa kuwa Tanzania ni moja ya nchi nne Afrika ambazo zimefanikiwa kupunguza vifo hivyo kwa zaidi ya asilimia 50.
“Hivi sasa tuna vifo vya watoto 54 kati ya vizazi hai 1,000, wakati miaka michache iliyopita vilikuwa vifo 102 kati ya vizazi 1,000,” alisema.
Akizungumzia kuhusu mashine za kuwahifadhi watoto njiti za incubator, Naibu waziri huyo anasema kuwa hivi sasa kuna njia bora zaidi kuliko hiyo.
“Kangaroo ni njia nzuri na hata hizo hospitali ambazo hazina incubator kuna njia mbadala wanaitumia,” alisema.
Sababu za mtoto kuzaliwa njiti
Kwa mujibu wa WHO, kuna sababu mbalimbali zinazosababisha mama mjamzito kujifungua mtoto njiti, ikiwa ni pamoja na kupata uchungu mapema kabla ya muda unaotakiwa.
WHO linasema historia inaonyesha kuwa kinamama wengi hujifungua mapema kutokana na kushika mimba mara kwa mara, maambukizi ya maradhi na kupatwa magonjwa sugu kama Kisukari na Shinikizo la damu, huku wengine wakilazimika kujifungua mapema baada ya kupata uchungu wa muda mrefu.
Dk Mtangi anataja sababu nyingine kuwa ni ukosefu wa lishe bora kwa kinamama wajawazito, wanawake kupata mimba wakiwa na miaka chini ya 18 au zaidi ya miaka 35 na matumizi ya pombe na sigara.
Aina tatu za watoto njiti
Shirika la Afya Duniani linasema kuna aina tatu za watoto wanaozaliwa njiti; kundi la kwanza ni wale ambao huzaliwa kabla ya wiki 28 (extreme preterm). Watoto wanaozaliwa katika kipindi hiki huhifadhiwa katika mashine maalumu (incubator), ambapo asilimia 90 ya watoto wanaozaliwa katika kundi hilo barani Afrika hufariki dunia.
Kundi la pili la watoto njiti huzaliwa kati ya wiki 28 na 32, ambapo huhitaji mashine kwa ajili ya kuwaongezea joto mwilini, ingawa pia husumbuliwa na magonjwa ya mfumo wa hewa kutokana na matatizo ya mapafu.
Kundi la mwisho la watoto njiti huzaliwa kati ya wiki 32 na 37, ambapo kati yao asilimia 60 ya vifo vya watoto hao hutokea barani Afrika.
Kwa mujibu wa Chuo cha Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi Tanzania (VETA), mashine ya ‘incubator’ inayoingizwa nchini hugharimu zaidi ya Sh6 milioni kwa moja huku mashine inayotengenezwa na chuo hicho, ambayo inatumia nishati ya umeme wa Jua inauzwa Sh3.5 milioni.
Akizungumza kwenye maonyesho ya Kilimo ya Nanenane, Dodoma, mwaka jana, mwalimu Emmanuel Bukuku alisema ingawa mashine hiyo ilikuwa haijapata ‘baraka’ zake kutoka wizarani kwa ajili ya kuanza kutumika kwenye hospitali nchini, zimeonyesha ufanisi ukubwa katika kuwahudumia watoto waliozaliwa kabla ya wakati.
Kwa mujibu wa takwimu za WHO zilizotolewa mwaka jana, nchi 10 zinazoongoza kwa vifo vingi vya watoto njiti duniani na idadi yake kwenye mabano ni India (3.5 milioni), China (1.1 milioni), Nigeria (773, 600), Pakistan (748, 100) na Indonesia (675, 700).
Nyingine ni Marekani (517, 400), Bangladesh (424, 100), Ufilipino (348, 900), Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo (DRC) (341 400), na Brazil (279 300).
Nyongeza na Joyce Joliga (Songea) na Rehema Matowo (Moshi).
|
0 Comments