Barker alisema Tanzania ina bahati kupata rasilimali hizo na kwamba zinaweza kubadilisha maisha ya wananchi kwa kuwaletea maendeleo makubwa iwapo tu hawataangalia historia ya migogoro iliyotokana na upatikanaji wa gesi na mafuta kwenye nchi nyingine za Afrika.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Tanzania imeshauriwa kutotishwa na migogoro mbalimbali baraniAfrika inayotokana na rasilimali za gesi na mafuta, badala yake ifuate mipango yake iliyojiwekea ili kuwanufaisha wananchi wote.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nishati na Mabadiliko ya Tabianchi wa Uingereza, Greg Barker katika mahojiano maalumu na mwandishi wetu nyumbani kwa Balozi wa nchi hiyo hapa nchini.
Barker alisema Tanzania ina bahati kupata rasilimali hizo na kwamba zinaweza kubadilisha maisha ya wananchi kwa kuwaletea maendeleo makubwa iwapo tu hawataangalia historia ya migogoro iliyotokana na upatikanaji wa gesi na mafuta kwenye nchi nyingine za Afrika.
Alisema ujio wa gesi nchini utalisaidia taifa kukabiliana na ongezeko la uharibifu wa mazingira kwa kuacha kukata miti kwa ajili ya mkaa na kuanza kutumia nishati hiyo.
Pia katika ziara hiyo iliyomkutanisha na Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge, Barker alitembelea mradi mkubwa wa umeme wa nishati ya upepo huko Singida utakaozalisha megawati 100 unaosimamiwa kwa ubia na Kampuni ya Aldwych ya Uingereza.
Waziri huyo aliimwagia sifa Tanzania kuwa imepiga hatua kuwa kupambana na ukosefu wa nishati kwa kuongeza uzalishaji kutoka asilimia 4.9 mpaka asilimia 14 kwa miaka mitatu... “Uingereza itafanya yote yanayowezekana kusaidia jitihada hizi.”
“Kwa kusaidia sekta ya nishati rafiki kwa mazingira Tanzania, Uingereza itafanya kazi kwa karibu… Hii ni muhimu kuhakikisha joto la wastani halitaongezeka juu ya nyuzi mbili zaidi ya viwango vya kabla ya viwanda,” alisema.
Balozi wa Uingereza nchini, Diana Melrose alisema Tanzania ina fursa kubwa ya kuimarika kiuchumi kutokana na rasilimali mbalimbali ilizonazo kwa kuwa inaungwa mkono wa mataifa makubwa.
|
0 Comments