Dar es Salaam. Watu watatu wamepora kiasi kikubwa cha fedha katika Benki ya Barclays, Tawi la Kinondoni, Dar es Salaam katika tukio linaloweza kufananishwa na sinema.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo lililotokea jana saa tatu asubuhi, watu hao wakiwa kwenye pikipiki moja walifika katika benki hiyo na kuiegesha nje ya uzio, kisha wawili kati yao wakiwa na silaha waliingia ndani.
Muda mfupi baadaye, walitoka nje wakiwa na mfuko mkubwa wenye fedha na lakini walipokuwa wakitaka kukimbia, mfuko huo ulianguka. Hata hivyo, waliuokota na kutokomea kusikojulikana.
Mmoja wa mashuhuda, Ali Lunde alisema: “Walitoka bila wasiwasi tena hawakupiga risasi wala kumtisha mtu yeyote. Walikuwa na mfuko mkubwa wa ‘kisalfeti’. Walipopanda pikipiki jamaa aliyebeba mfuko aliukumbatia kama amepakata mtoto.”
Lunde alisema wakati watu hao wakiondoka na pikipiki, baadhi ya wafanyakazi wa benki walitoka nje huku wakipiga kelele kuwa wamevamiwa na majambazi.
“Walitoka nje wakipiga kelele, ndipo kila mtu akajua walikuwa ni majambazi, kama watu wangekuwa na silaha wangeweza kuwadhibiti maana wote tuliokuwa hapa tumewaona wanavyoondoka,” alisema.
Dereva teksi anayeegesha gari lake karibu na benki hiyo, Herode Munyi alisema aliwashuhudia majambazi hao wakiingia kwenye benki wakiwa na silaha mkononi, jambo lililomfanya kuwapa taarifa watu wengine huku akitafuta namba za polisi.
“Baadaye nilifanikiwa kuwaona polisi hawa wanaotembea na pikipiki nikawaambia lakini kama vile walipitiliza, hawakwenda moja kwa moja benki,” alisema Munyi.
Hata hivyo, mashuhuda wa tukio hilo walionekana kushangazwa na mazingira ya wizi huo, kwani walisema mlinzi wa benki hiyo hakuwa na bunduki wala kirungu chochote wakati majambazi walipovamia.
Mmoja wa mashuhuda ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema wakati majambazi wanavamia benki hiyo, hakukuwa na watu wengi waliokuwamo ndani, jambo lililowapa urahisi wa kutekeleza dhamira yao.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura alisema tawi hilo la benki halina polisi wanaolinda baada ya benki hiyo kuwaondoa hofu kwa madai kuwa halina biashara kubwa.
“Mwaka 2012/2013 waliondoa polisi katika benki ambazo hazina biashara kubwa ikiwamo hii, lakini kuna haja ya kurudisha ulinzi wa askari polisi,” alisema Wambura.Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa Barclays, Neema Singo alikana madai hayo akisema benki yake ina mkataba na jeshi hilo pamoja na ile yaUltimate Security na kusema wameshangaa kwamba polisi hawakuwapo wakati tukio hilo lilipotokea.
“Tuna mkataba na polisi wa kulinda matawi yote. Tunachunguza nini kimetokea,” alisema Singo na kuongeza kwamba kutokana na tukio hilo, tawi hili litafungwa wakati uchunguzi wa polisi ukiendelea.
Kamanda Wambura alisema kiwango cha fedha kilichoibwa bado hakijafahamika na kwamba hesabu zilikuwa zikiendelea kufanywa, huku juhudi za kuwatafuta wezi hao zikiendea.
“Hakuna aliyejeruhiwa ingawa mfanyakazi mmoja amepelekwa hospitali kutokana na mshtuko,” alisema Wambura.
Mwandishi aliwashuhudia baadhi yawafanyakazi wa benki hiyo wakiwa wamelala kwenye gari la wagonjwa wakipatiwa msaada baada ya kupata mshtuko. Pia polisi walionekana wakizunguka eneo hilo huku wakiwahoji baadhi ya wafanyakazi.
|
0 Comments