Wema na Kajala wapo kwenye gogoro zito kwa muda mrefu huku mashabiki wa mastaa hao waliojipa majina ya Team Wema (wanaomuunga mkono Wema) na Team Kajala (walio upande wa Kajala) wakiukuza ugomvi huo kwa kushambuliana kwa maneno makali kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
WEMA KUFUNGUKA
Katika gazeti hili, toleo namba 877 la Aprili 25-Mei Mosi, 2014 la wiki iliyopita, liliandika habari ya Wema iliyokuwa na kichwa; Kwa mara ya kwanza Wema afunguka, asema: NAJUTA KUMLIPIA KAJALA MIL. 13! Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Wema kufunguka baada ya bifu la kimyakimya la muda mrefu ambapo alifafanua chanzo cha bifu lao na namna anavyojuta kumlipia Kajala fedha hizo.“Kusema kweli najuta kumlipia (Kajala) ile faini ya Sh. milioni 13. Bora angeenda jela miaka saba kuliko kunisababishia matatizo na maumivu kiasi hiki. Mimi sijawahi kumsema vibaya K kisa eti nilimlipia fedha hizo,” alisema Wema katika gazeti hilo. Alipoambiwa kama Kajala yupo tayari kurudisha fedha hizo alisema: “Kama anataka kunilipa, anilipe kisha aende jela maana mimi sikumkopesha, nilitoa kwa moyo.”
HABARI ZA MOTO
Baada ya gazeti hilo kuruka mitaani na Kajala kulipata ndipo akaeleza mambo mazito. Akizungumza na mwanahabari wetu, Kajala alisema katika vitu ambavyo Wema anatakiwa kuvisahau ni pamoja na kumlipia mahakamani hizo milioni 13. “Siwezi kumlipa ng’o. Namlipa nini sasa na kivipi? Kwani tulikopeshana? Hakuna anachonidai Wema, hata kama akisema nimlipe, siwezi kufanya hivyo,” alisema Kajala.Huku akimwaga machozi, Kajala aliendelea: “Unajua haya mambo yanachukuliwa kirahisi tu na wadandiaji wa mambo, ni vile watu hawajui ni kwa kiwango gani hili suala linaniumiza. “Wema alinisaidia, alinilipia fedha mahakamani wakati ambao nilikuwa na uhitaji na sikuwa na zile fedha. Kama asingejitokeza kunilipia nilikuwa nakwenda jela. “Lile ni jambo kubwa. Thamani yake haifananishiki na fedha. Ule ulikuwa ni utu tu, sasa leo iweje ligeuzwe kuwa kama deni? Siwezi kufanya hivyo.”
UPO TAYARI KWA SULUHU
Kwa mara nyingine tena, Kajala alisema kuhusu kupatana na Wema yupo tayari muda wowote, maana haoni sababu ya kuendelea kwa ugomvi huo. Hii ni mara ya tatu Kajala kuzungumzia suluhu akisisitiza: “Nakosa amani kabisa na huu mzigo. Natamani kuutua. Nipo tayari kukutanishwa naye hata leo tuyamalize.”
HABARI YA MJINI
Habari ambazo zimeenea mjini lakini bado hazijathibitishwa zinadai kuwa, Kajala anajiamini kwa sababu anajua fedha alizolipiwa na Wema si zake, zililipwa na aliyekuwa mwanaume (boyfriend) wa Wema, yule kigogo wa Ikulu anayetajwa kwa jina la CK. “Lile lilikuwa agizo, Wema hakuwa na fedha zote zile kwa ajili ya kumlipia Kajala. Alipewa na CK na kuambiwa amlipie ili asiende jela,” alisema mmoja wa watu wa karibu na mastaa hao kwa sharti la kutotajwa gazetini.
0 Comments