Mlipuko umetokea katika kituo cha basi
Wafanyikazi wa shughuli za uokoaji katika mji mkuu wa Nigeria Abuja wanasema kuwa zaidi ya watu tisa wameuwawa katika mlipuko uliotokea karibu na kituo cha basi. Mlipuko huo umetokea karibu na eneo ambako kulitokea shambulizi baya la bomu mwezi uliopita.Mlipuko huo umetokea katika eneo la Nyanya, karibu na kituo cha basi ambako zaidi ya watu sabini waliuwawa katika shambulizi la tarehe14 mwezi Aprili. Ripoti za awali zimesema kuwa watu kadhaa wameuwawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Waandishi wanasema kuwa mlipuko huo umesababishwa na bomu lililotegwa ndani ya gari. Mmoja wa walioshuhudia kisa hicho amesema aliona miili 20 ya watu waliouwawa. Hakuna kundi lililodai kuhusika katika shambulizi hilo lakini kundi la wanamgambo wa kiislamu la Boko Haram limewahi kutekeleza mashambulizi kama hayo mjini Abuja.

Mengi ya mashambulizi ya Boko Haram yamekuwa yakitokea katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria. Lakini shambulizi la bomu la tarehe 14 Aprili lilizua hofu kwamba huenda wanamgambo hao wameanza kupanua maeneo wanayoendeleza harakati zao.