Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Tanzania Mh:Bernad Membe |
Dodoma/Dar es Salaam.
Siku chache baada ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Maselle kutaka Balozi wa Uingereza nchini Dianne Melrose, ajipime kwa kile kinachodaiwa kuingilia mambo ya ndani ya nchi, Serikali imemsafisha balozi huyo ikisema imeshalimaliza suala hilo.
“Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa ufafanuzi kidogo kuhusu jambo hili ambalo sote tunalifahamu kuwa liliibuka hapa bungeni, ni kweli nilimwagiza Waziri Membe na akafanya kazi ya kuwakutanisha na kuwasuluhisha wawili hawa na kwa kweli walishalimaliza kwa hiyo naomba tusiliendeleze tena,” alisema Pinda.
Alitoa kauli hiyo kutokana na mwongozo ulioombwa na mbunge wa Viti Maalumu, Suzana Lyimo aliyetaka kauli ya Serikali kuhusu tuhuma dhidi ya balozi huyo nchini Tanzania.
Akizungumza katika sherehe za siku ya kuzaliwa ya Malkia Elizabeth wa Uingereza zilizofanyika nyumbani kwa balozi huyo Dar es Salaam hivi karibuni, Waziri Membe alisema hakuna mgogoro wowote wa kidiplomasia utakaowekwa na Tanzania dhidi ya balozi huyo kutokana na uhusiano wa kina uliopo baina ya nchi hizo mbili.
“Tumeshatuma watu nchini Uingereza kupeleka masikitiko yetu na kuomba radhi kutokana na kauli iliyotolewa bungeni. Hii ni kutokana na uhusiano mzuri tulionao Uingereza na Tanzania na hatutaki kuuharibu uhusiano huo,” alisema Membe.
Membe alisema kwa kuwa Serikali haipo tayari kuharibu uhusiano kati ya nchi hizo mbili, Waziri Mkuu Mizengo Pinda atalizungumzia suala hilo hivi karibuni bungeni, ili kumhakikishia balozi huyo kuwa hana tuhuma za kujibu.
Mei 30 mwaka huu, Waziri Maselle alimlipua balozi huyo wakati akichangia hoja iliyotolewa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila(NCCR-Mageuzi) bungeni iliyoihusisha Uingereza na urejeshwaji wa Sh76 bilioni za chenji ya Rada.
Akichangia hoja hiyo, Maselle alimshutumu Balozi wa Uingereza kuhusika na kuratibu vikao jijini Dar es Salaam na Dodoma kinyume cha taratibu na hadhi ya kidiplomasia.
Alidai kuwa balozi huyo amekuwa akihusika katika kusambaza ujumbe mfupi unaodaiwa kutaka kukwamisha Bajeti ya Nishati na Madini pamoja na kuwashawishi marafiki wa kimaendeleo wasitishe misaada ya kibajeti kwa Tanzania.
Katika maelezo yake, Membe alisema tuhuma zilizotolewa hazina ukweli wowote na ni lazima zitolewe ufafanuzi ndani ya Bunge ili kudumisha urafiki wa nchi hizo mbili.
“Kama kauli hiyo ilivyotolewa bungeni kumshutumu balozi, hali kadhalika tutahakikisha tunaomba msamaha kwa kile kilichotamkwa dhidi ya balozi. Uchunguzi umefanyika na tumegundua kuwa hakuna tuhuma zozote zenye ukweli dhidi yake,” alisema.Alifafanua kuwa uhusiano kati ya Uingereza ni mzuri na ndiyo maana kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa Rais Jakaya Kikwete ameshakwenda nchini humo zaidi ya mara nne kwa shughuli za kudumisha umoja na ushirikiano.
Membe alisema, Uingereza imekuwa mwekezaji mzuri hasa katika masuala ya nishati ya gesi, miundombinu, Ukimwi na afya.
Gazeti hili lilizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Siasa, Miradi na Habari wa Ubalozi, Tamsin Clayton kutaka kujua msimamo wa ubalozi huo kuhusu kauli ya Maselle na ile ya Membe, lakini aliahidi kuzungumza na balozi ili kutolea ufafanuzi kadhia hiyo.
Hata hivyo, Ofisa Miradi na Habari wa Ubalozi, Michael Dalali alisema Membe alizungumza hayo wakati wa sherehe za kuzaliwa za Malkia wa Uingereza na kuweka bayana uhusiano mzuri uliopo kati ya Uingereza na Tanzania.
Maselle alisema licha ya kuwa wanadiplomasia wana kinga ya kutokushtakiwa lakini wanatakiwa kuheshimu sheria za nchi na kanuni zake na pia alimtaka balozi huyo kujipima kama anafaa na anatosha kuiwakilisha nchi yake hapa Tanzania.
0 Comments