Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alihutubia taifa Jumanne akisisitiza kuwa ana imani kuwa mashambulio hayo yalichochewa kisiasa.
Ametoa matamshi hayo licha ya taarifa kutoka kwa kundi la wapiganaji wa kiislamu wa AL shabaab waliodai kuwa wao ndio waliohusika.
Acha kutukejeli - upinzani
Matamshi ya rais Kenyatta yame kejeliwa na wanasiasa wa upinzani nchini humo waliodai kuwa rais huyo hana ufahamu wa yale yanayoendelea nchini mwake.
Seneta kutoka chama kikuu cha upinzani, Moses Wetangula amesema matamshi ya rais sio ya kweli. '' Badala ya kuitisha usaidizi wa wenzetu wenye teknolojia bora, hata tutumie ndege zisizo na rubani kuwalipua huko waliko, tunakaa hapa Nairobi na kudai AL shabaab hawakuhusika.'' Wetangula aliambia bunge la Kenya. '' Huu ni mzaha,'' Aliongeza bwana Wetangula.
Lakini uchunguzi uliofanywa na BBC umeonesha kuwa huenda kuna uzito kwa madai ya rais Kenyatta.
Wakaazi wengi wa Mpeketoni waliozungumza na BBC wametueleza kuwa, wanaamini shambulio la Jumapili usiku linatokana na mzozo wa ardhi kati ya jamii zinazoishi huko.
Wakaazi hao wamesema kuwa Al shabaab wamedakia tu kujigamba kwa yaliotokea huko ila wao wanaamini kuwa ni jambo lililokuwa likitokota kwa muda mrefu.Huku hayo yakiarifiwa, polisi wanasemekana kuimarisha doria katika eneo la Lamu na vitongoji vyake. Wanajeshi wachache wametumika kuimarisha usalama hasa katika kijiji cha Mpeketoni.
Katika taarifa zilizotufikia ni kuwa Polisi wameimarisha usalama katika mkoa wa magharibi mwa Kenya kutokana na duru walizopokea kuwa huenda eneo hilo likalengwa kwa shambulio.
Al shabaab wamefanya mashambulio ya mara kwa mara katika sehemu mbali mbali nchini Kenya tangu majeshi ya Kenya yaingie nchini Somalia mwaka wa 2011, katika oparesheni ya kuwafagia kutoka nchini humo.
Shambulio la punde zaidi linadaiwa kufanywa kama kulipiza kisasi ya kuuawa kwa masheikh 2 wa kiislamu katika mji wa Mombasa pwani ya Kenya hivi majuzi.
|
0 Comments