|
Wafanyakazi wa BBC wakiwa kazini kupeperusha matangazo ya Dira ya Dunia redio
Idhaa ya kiswahili ya BBC imezindua rasmi studio zake mjini Dar es Salaam kwa mbwembwe na haiba kuu.
Uzinduzi huo ni matokeo ya mkakati na uwekezaji wa miaka mingi wa shirika la BBC duniani kuhakikisha kuwa matangazo yake yanawafikia wasikilizaji katika hali ya ubora wa hali ya juu na ya kisasa zaidi.Katika hafla hiyo iliyoandaliwa katika ofisi hizo hizo mpya zilizoko eneo la Mikocheni, mkuu wa kitengo cha uandishi wa habari katika BBC, Nicki Clarke, ameshukuru serikali ya Tanzania, kwa kuwaruhusu kujenga studio hizo za kisasa zitakazoinua tasnia ya habari nchini humo na uhuru wa habari kwa ujumla.
Naye mkuu wa ofizi ya Dar es Salaam, Hassan Mhelela mbali na kuwataka wafanyakazi wa BBC Tanzania, kuzidi kuonyesha ushirikiano pamoja na utendaji kazi wa pamoja, pia ametangaza kuanishwa rasmi kwa ushirikiano kati ya BBC na chuo kikuu cha Dar es Salaam kitengo cha uandishi wa habari.
|
Ushirikiano huo amesema kuwa unalenga kusaidia kutoa mafunzo kwa wandishi wa habari chipukizi walioko mafunzoni katika chuo hicho, ambao kwa nyakati tofauti, watakuwa wakijiunga na BBC ili kupata mafunzo katika uandaaji vipindi vya redio na televisheni pamoja na utangazaji.
Kwa upande wa BBC, kuanzishwa kwa ofisi hii, yenye studio za kisasa kabisa za redio na televisheni mbali na kuongeza ubora wa vipindi lakini pia kutawezesha matangazo ya redio na televisheni kufanyika moja kwa moja kutokea Dar es Salaam.
Na kuanzia sasa matangazo ya Amka na BBC yatakuwa yakiandaliwa Dar es Salaam.
Itakumbukwa kuwa Tanzania mbali na kuwa na wasikilizaji wengi wa idhaa ya kiswahili ya BBC, lakini pia ndiko kunakozungumzwa zaidi lugha ya kiswahili.
Tanzania pia ina rekodi ambapo mtangazaji wa kwanza au sauti ya kwanza iliyosikika mwaka 1957, ilikuwa ya mtanzania Oscar Kambona ambapo alikuwa mwanafunzi mjini London.
0 Comments