Afisa mkuu wa umoja wa Ulaya EU Jose Manuel Barroso amemtahadharisha rais wa Urusi Vladimir Putin dhidi ya kutuma majeshi yake nchini ukraine kwa kisingizio chochote kile.
Mazungumzo hayo yalifuatia tangazo la Kremlin kuwa inapanga mikakati ya kutuma misaada ya kibinidamu mashariki mwa Ukraine kwa ushirikiano na shirika la Msalaba mwekundu.Katibu mkuu wa muungano wa Nato Anders Fogh Rasmussen ameishtumu Urusi kwa kusingizia msaada wa kibinadamu ilikuingilia kati kijeshi mashariki mwa Ukraine.
Msalaba mwekundu haujatoa taarifa ya aina yeyote hadi kufikia sasa.
Takriban watu 1,500 wameuawa baada ya serikali ya Kiev kutuma majeshi yake mashariki mwa taifa hilo katika miji ya Donetsk na Luhansk ili kukabiliana na waasi wanaounga mkono kujiunga na Urusi.Makumi ya Maelfu ya watu wametorokea Urusi tangu makabiliano haya yaanze mwezi Aprili mwaka huu.
Duru zinaarifu kuwa majeshi ya Ukraine yamezunguka mji wa Donetsk, mji wenye zaidi ya wakaazi milioni moja na ambao katika siku za hivi punde umekuwa bila umeme na bidhaa muhimu kama chakula na madawa.
Haijajulikana hadi sasa msaada huo na msafara utaondoka lini kuingia Ukraine.Serikali ya Kiev inahofia kuwa msaada huo utakuwa kisingizio cha Urusi kuingiza silaha za kuwahami waasi ambao wanapigana wakitaka kujiunga na Urusi.
Bwana Barroso alizungumza na rais wa Ukraine Petro Poroshenko ilikujadili hali halisi katika mji wa Luhansk.
|
0 Comments