Kwa maana hiyo Bunge, hilo linatumia Dola 5,400 sawa na Sh8.91 milioni kwa siku kugharimia vipaza sauti katika vyumba 12 vinavyotumiwa na kamati hizo na kwa siku 16 ambazo kamati zitakutana, gharama hizo zitafikia Sh142.56
Dodoma. Wakati kukiwa na malalamiko kwamba Bunge la Maalumu la Katiba linagharimu fedha nyingi za walipakodi, uongozi wa taasisi hiyo umetumia Sh142.56 milioni kukodi vipaza sauti kutoka Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alithibitisha kukodiwa kwa vipaza sauti hivyo kwa ajili kamati zote 12 na kwamba kila gharama ya chumba kimoja kwa siku ni Dola 450 za Marekani (Dola moja ni wastani wa Sh1,650).
Kwa maana hiyo Bunge, hilo linatumia Dola 5,400 sawa na Sh8.91 milioni kwa siku kugharimia vipaza sauti katika vyumba 12 vinavyotumiwa na kamati hizo na kwa siku 16 ambazo kamati zitakutana, gharama hizo zitafikia Sh142.56.
“Vifaa vya sauti tulivyokuwa navyo vinalalamikiwa, vilikuwa siyo standard (viwango) hasa vya mazungumzo, tumekodi kutoka Ukumbi wa Mikutano wa AICC na tumekuwa nao usiku mzima kuvifunga,” alisema.
Alisema tangu wavifunge, hawajawahi kupata malalamiko tena kutoka katika kamati kuhusu ubora na kwamba gharama za kukodisha vifaa hivyo itatoka katika fungu la dharura la Bunge Maalumu.
“Mara ya kwanza walituambia gharama zao ni Dola 500 kwa siku lakini tukajadiliana nao, hivyo tukafikia kiwango hicho cha Dola 450,” alisema.
Hamad alisema vifaa vya awali ambavyo vililalamikiwa na wajumbe kuwa havitoshi, vinatoa sauti nje ya majengo na kwa jinsi vilivyo, vinalazimika kutembezwa ukumbini, hivyo kusababisha usumbufu.
Suala la gharama limekuwa likiibuka mara kwa mara na wakati mwingine kutajwa kama sababu ya kuahirishwa kwa Bunge hilo kwa kuwa hakuna uhakika wa kupatikana kwa akidi inayotakiwa kufikia uamuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alilalamikia kile alichokiita “matumizi ya kufuru” ya Bunge Maalumu wakati hakuna uhakika wa kupatikana kwa Katiba Mpya.
Kibamba alisema ikiwa Bunge litaendelea na vikao vyake hadi Oktoba 31, mwaka huu kama ratiba inavyoonyesha, sehemu hiyo ya mchakato itakuwa imeligharimu taifa Sh40 bilioni, fedha ambazo zingetosha kugharimia maji kwa wananchi wote wa Wilaya za Kondoa mkoani Dodoma na Kilindi, Tanga.
“Tatizo kubwa hapa ni posho, kila mara sheria na kanuni zimekuwa zikibadilishwa ili kuongeza muda wa Bunge siyo kwa ajili ya kitu kingine, bali kwa ajili ya posho, kwa hiyo gharama zinazidi kuongezeka na haya ni matumizi ya kufuru ambayo hayapaswi kufanywa katika nchi maskini kama yetu,” alisema Kibamba na kuongeza:“Katika awamu ya kwanza, zaidi ya Sh10 bilioni zilitumika na sasa fedha zilizotengwa kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Fedha (Mwigulu Nchemba) ni Sh20 bilioni na hizo zilitengwa kwa siku 60 tu lakini kwa siku zilizoongezwa hadi kufikia kati ya 84 na 90, gharama zitaongezeka kwa zaidi ya Sh10 bilioni.”
Katika hatua nyingine, Bunge Maalumu linakusudia kuajiri wataalamu 10 kutoka nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi ili kusaidia utekelezaji wa majukumu yake.
Hamad alisema ulazima huo unatokana haja ya kupata watu wa kusaidia kwenye kamati na kwenye uandishi.
|
0 Comments