Wakuu wa serikali na mashirika mbali mbali wanaohudhuria mkutano wa umoja wa mataifa unaoendelea mjini New York leo walijadili hatma ya taifa la Somalia ambalo linajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka 2016.
Akizunguma wakati wa kikao hicho, mwenyekiti wa tume ya muungano wa Afrika Bi, Nkosazana Dlamini Zuma, aliambia kikao hicho kuwa serikali ya sasa ya Somalia imefikia maendeleo makubwa katika harakati za kurejesha amani na utawala wa sheria, licha ya changamoto nyingi zinazoikumba kama vile kutokomeza kundi la Kiislamu ya Al Shabaab.
Akihutubia mkutano wa umoja wa mataifa mjini New York, Bi Zuma alisema juhudi za kubuniwa kwa serikali za majimbo nchini humo na kushirikishwa kwa taasisi zote za kisiasa na umoja wa serikali, idara ya mahakama na bunge zimechangia pakubwa kuimarisha hali ya maisha nchini Humo.
Hata hivyo alisema wanawake wana nafasi kubwa katika kuchangia amani na uchumi wa Somalia na hivyo wanapaswa kushirikishwa katika harakati hizo.
Wakati huo huo amesema ni sharti miji iliyosalia chini ya wapiganaji wa Al Shabaab yakombolewe ili amani iweze kupatikana nchini Somalia, na kuonya kuwa endapo taasisi zilizoko hazitalindwa hali nchini Somalia huenda ikawa mbaya zaidi.Aidha amesema raia wengi wa Somalia wanahitaji misaada ya dharura na huduma zingine kama vile elimu, afya na maji.
Amekariri kuwa muungano wa Afrika utaendelea na operesheni ya pamoja na jeshi la Somalia ili kukomboa miji inayodhibitiwa na wapiganaji wa Al -Shabaab.
Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kusadia jeshi la serikali ya Somalia kwa mafunzo na vifaa ili liweze kuendeleza harakati za kulinda amani wakati wanajeshi wa muungano wa Afrika watakapoondoka.
Kuhusiana na madai, yaliyochapishwa na shirika la Human Rights watch, kuwa wanajeshi wa Muungano huo wanaohudumu nchini Somalia AMISOM, wanawadhulumu wanawake, Bi. Zuma amesema Muungano wa afrika umeanzisha uchunguzi, ili kuthibitisha madai hayo na kusema wanajeshi wa muungano huo watakaopatikana na hatia watachukuliwa hatua za kisheria.
Shirika hilo la Human rights watch lilichapisha habari kudai kuwa wanawake na wasichana wengi nchini Somalia wamedhulumiwa kimapenzi na wanajeshi hao wa AMISOM.
Ripoti hiyo ilinadi kuwa wanajeshi hao pia hutumia vyakula vya misaada kama mtego wa kuwadhulumu kina mama na hata mara nyingine fedha walizo nazo, na hivyo kukiuka maadili ya utendaji kazi.
|
0 Comments