Jamhuri ya Demokrasi ya Congo imejitangaza kuwa haina tena virusi vya ebola baada ya virusi kuambukiza watu kwa miezi mitatu na kuuwa wagonjwa karibu 50.
Virusi vya Ebola vilivyoathiri Congo ni tofauti na vile vya Afrika Magharibi.
Lakini Waziri wa Afya, Felix Kabange Numbi, amewasihi watu bado kuwa macho - kwamba kumalizika kwa ugonjwa, haimaanishi kuwa nchi haiko kabisa hatarini.
Na Daktari wa Sierra Leone ambaye ameambukizwa Ebola amepelekwa Marekani kwa matibabu.
Martin Salia, ambaye ana kibali cha makaazi Marekani na ambaye ameoa Mmarekani, atatibiwa wakati ametengwa kwenye kitengo maalumu katika jimbo la Nebraska.
Haijulikani iwapo Dr Salia, daktari wa upasuaji, aliuguza wagonjwa wa Ebola Sierra Leone.
Hospitali alikofanya kazi haina kituo cha kuuguza wagonjwa kama hao.
Dakta Salia atakuwa mgonjwa wa 10 wa Ebola kuuguzwa Marekani.
Hadi sasa watu zaidi ya 5,000 wamekufa kutokana na Ebola Afrika Magharibi.
Juma hili iliripotiwa kwamba wakati idadi ya maambukizi ya Ebola yanapungua Liberia na Guinea, bado yanaongezeka nchini Sierra Leone.
Na katika tukio jengine, Ufaransa imewashauri raia wake wasiende katika sehemu fulani za Mali baada ya watu watatu kufariki huko kwa sababu ya Ebola.
Raia wa Ufaransa walioko Mali wameambiwa wafuate ushauri wa serikali ya Mali.
|
0 Comments