Luteni Kanali Isaac Zida
Jeshi nchini Burkina Faso limeahidi kuunda serikali ya umoja ili kusimamia mchakato wa kisiasa, baada ya maandamano makubwa yaliyomlazimisha Rais Blaise Compaore kujiuzulu wiki iliyopita.Msemaji wa serikali amesema haina maana kwa jeshi kubakia madarakani na litaendelea kuzungumza na upinzani, viongozi wa dini na mabalozi wa kimataifa siku ya Jumatatu.
Hatua hii ya jeshi imekuja wakati maelfu ya waandamanaji katika mji mkuu wa Ouagadougou wakitaka jeshi liachie madaraka.

Mwaandamanaji mmoja ameuawa katika mapigano ya Jumapili.
Umoja wa Mataifa umelaani jeshi kutwaa madaraka nchini Burkina Faso na kutishia kuwawekea vikwazo.Kiongozi wa muda mrefu Bwana Compaore alijiuzulu Alhamisi, kufuatia maandamano ya siku kadhaa ya kuipinga serikali.
Jeshi lilimtangaza Luteni Kanali Isaac Zida siku ya Jumamosi kuwa kiongozi wa serikali ya mpito.
Hata hivyo maelfu ya waandamanaji walikusanyika Jumapili katika mji mkuu Ouagadougou, wakipinga hatua ya jeshi la nchi hiyo kutwaa madaraka.
Jumapili jioni, kufuatia mkutano na viongozi muhimu wa upinzani, msemaji wa jeshi amesema jeshi litaunda serikali ya mpito ikiwa na mambo yote muhimu yatakayokubalika na wengi.
"Madaraka si kipaumbele chetu, ila tu kwa manufaa makubwa zaidi kwa taifa," imesema taarifa ya jeshi.
Mwaandamanaji mmoja alibeba bango lililosomeka kuwa "Zida Ondoka" wakati wa mkutano wa hadhara katika bustani kuu ya Ouagadougou.
Lilikuwa jambo linalohitajika kuwatawanya waandamanaji ili "kuleta utulivu", imesema taarifa hiyo ya jeshi, ikiongeza kuwa mwaandamanaji mmoja nje ya kituo cha televisheni ya taifa aliuawa.Kulikuwa na hali ya wasiwasi katika makao makuu ya televisheni ya serikali Jumapili, wakati kiongozi wa upinzani Saran Sereme na waziri wa ulinzi wa zamani Kwame Lougue walipofika katika mkutano.
Inaaminika kuwa kila mmoja wao alikwenda hapo kutangaza kuwa angeweza kuongoza serikali ya mpito.
Hata hivyo muda mfupi baada ya kuwasili hapo, risasi zilianza kufyatuliwa, ambapo wafanyakazi wa kituo hicho na waandamanaji walikimbia.
Watu walioshuhudia tukio hilo wameiambia BBC kuwa askari walifyatua risasi hewani ili kuwatawanya waandamanaji kabla ya kuwalazimisha waandishi wa habari kuondoka eneo hilo.
Televisheni ya taifa ilirejesha matangazo yake baada ya saa chache baadaye.
Majeshi pia yaliwaondoa waandamanaji kutoka katika bustani kuu ya mjini Ouagadougou, iitwayo Place de la Nation.