Mtaalam Mwelekezi kutoka Kampuni ya Petrogas Bw. Tom Mitro (kushoto) akielekeza namna ya kuandaa mapendekezo ya miradi ( project proposals) mbele ya washiriki wa mafunzo hayo.
Baadhi ya washiriki kutoka Wizara ya Nishati na Madini wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zinawasilishwa na Bw. Tim Mitro kutoka kampuni ya Petrogas(hayupo pichani).

Mtaalam Mwelekezi kutoka Kampuni ya Petrogas Bw. Tom Mitro akisisitiza jambo wakati wa mafunzo hayo.
Na Greyson Mwase, Bagamoyo

Wataalamu wa Nishati na Madini wametakiwa kushirikisha jamii inayozunguka
miradi inayoanzishwa ili kuzuia migogoro inayoweza kutokea kutokana na wananchi
kukosa uelewa na miradi mipya.

Wito huo umetolewa na mtaalamu kutoka kampuni ya Petrogas Bw. Tom Mitro katika mafunzo ya jinsi ya kuandaa mapendekezo ya miradi, sera pamoja na utekelezaji wake yanayoendelea mjini Bagamoyo. Mafunzo hayo yalishirikisha
wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Nchini,

(TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TDGC).

Bw. Mitro alisema kuwa katika nchi nyingi za Afrika hususan zenye rasilimali nyingi 


kumekuwepo na migogoro mikubwa katika uanzishwaji wa miradi kutokana na jamii kutoshirikishwa kabla ya kuanzishwa kwa miradi.

Alisema katika hatua za awali za maandalizi ya miradi, wadau mbalimbali

muhimu wamekuwa wakishirikishwa ikiwa ni pamoja na taasisi za kifedha, serikali,

wanasiasa, wahisani huku kundi la jamii inayozunguka miradi husika likisahauliwa

kabisa.

Akielezea athari za kutowashirikisha jamii inayozunguka miradi Bw. Mitro alisema

kuwa ni pamoja na migogoro inayopelekea kukwama kwa miradi hali inayopelekea

miradi kutokamilika kwa wakati.

“ Wananchi wengi wanapokosa uelewa wa miradi yenye manufaa kwa taifa, matokeo

yake ni kuipinga hali inayopelekea kukwama kwa miradi hiyo.” Alisema Bw. Mitro.

Bw. Mitro alisema kuwa jamii inayozunguka miradi pamoja na asasi za kiraia zina

umuhimu mkubwa sana katika ushirikishwaji katika uanzishaji wa miradi kwani ndio

walinzi wa miradi husika hususan miundombinu yake.

Akilelezea jinsi jamii inayozunguka miradi inavyoweza kushirikishwa Bw. Mitro

alieleza kuwa ni pamoja na mikutano ya mara kwa mara na wananchi ikiwa ni

pamoja na wawakilishi wao na kusisitiza kuwa wanaposhirikishwa katika kila hatua

ya mradi wanakuwa mabalozi kwa wananchi wenzao.

Aliongeza kuwa ushirikishwaji wa jamii unaifanya jamii kuwa sehemu ya umiliki wa

miradi na kulinda miundombinu yake.

Mafunzo hayo yameandaliwa na mradi unaohusika na kuwajengea uwezo

wataalamu wa nishati na tasnia ya uziduaji (CADESE; Capacity Development

in the Energy Sector & Extractive Industries) lengo likiwa ni kuwajengea uwezo

wataalamu kutoka sekta za nishati na madini katika uandaaji wa mapendekezo

ya miradi mbalimbali ( project proposals) na sera na hivyo kuepusha gharama ya

kutumia wataalamu kutoka nje na kukuza umiliki

Mafunzo hayo yatakayochukua wiki tatu yatashirikisha washiriki 60 ambapo kila

kundi la washiriki 20 litajifunza kwa muda wa wiki moja. Kundi la kwanza litajifunza

juu ya uandaaji wa mapendekezo ya miradi na kufanya tathmini yake ( project

proposals preparations and evaluations ), kundi la pili litajifunza juu ya uandaaji wa

sera na kundi la tatu litajifunza juu ya usimamizi wa miradi.





Mradi wa CADESE unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika

na Maendeleo (UNDP) ulianzishwa mwaka huu unatekelezwa na Wizara ya Nishati

na Madini kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile Wakala wa Nishati Vijijini

(REA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Taasisi ya Uogozi na Taasisi

ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF).