Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ipanue wigo wa utoaji huduma za msingi kwa kuishirikisha zaidi sekta binafsi nchini.
 
“Ninawasihi waziri wa afya na naibu wake kwa vile ni wapya bado wabadili mtizamo wa wizara hii kwa kushirikisha zaidi wadau wa sekta binafsi kwenye utoaji wa huduma ili wasaidie kupunguza mzigo mkubwa ilionao serikali,” alisema.
 
Alitoa kauli hiyo wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa Sekta ya Afya wa mwaka 2014 ulioanza jana kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
 
Pinda aliyefungua mkutano huo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, alisema: “Kuna tatizo la kukumbatia utoaji wa huduma ... tunazo hospitali kubwa za wilaya zinazomilikiwa na taasisi za dini. Hivi ni kwa nini kama Wizara msiwasaidie kuwahudumia watumishi wao au kuwapa ruzuku kwenye dawa ili kuwawezesha kutoa huduma kwa ufanisi zaidi?,” alihoji Waziri Mkuu na kushangiliwa na washiriki wa mkutano huo.
 
“Hata ukiangalia takwimu kwenye utoaji wa huduma za afya kupitia mifumo ya bima ya afya utabaini kuwa ni asilimia 18 tu ya wananchi wanatumia bima ya afya na kati ya hao, asilimia 15.3 ni mifuko ambayo imeanzishwa na Serikali. Ni kwa nini basi msiwasaidie wadau wa sekta binafsi ili wachangie huduma hii na idadi wa watumiaji wa mfumo huu iongezeke haraka,” alihoji.
 
Akizumgumzia kuhusu uwiano kati ya daktari na mgonjwa, Waziri Mkuu alisema uwiano uliopo ni mbaya na kwamba hakuna njia ya haraka ya kupunguza tatizo hilo isipokuwa kwa kuishirikisha sekta binafsi kwenye ujenzi wa vyuo vikuu vya elimu ya tiba na sayansi za jamii.
 
“Uwiano wa sasa hapa nchini ni daktari mmoja kwa wagonjwa 75,000 wakati viwango vya kimataifa vinataka daktari mmoja awahudumie wagonjwa 7,000. Kwa wauguzi, hapa nchini muuguzi mmoja anahudumia wagonjwa 6,000 wakati viwango vya kimataifa vinataka muuguzi mmoja ahudumie wagonjwa 500,” alisema.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kudhibiti ugonjwa wa ebola kwenye vituo vya mipakani na kwenye viwanja wa ndege.