Wafanyabiashara wa soko la Machinga Complex Jijini Dar es Salaam, wamepata hasara ya mamilioni ya  fedha baada ya mali zao kuteketea kwa moto katika jengo hilo. 
 
Moto huo ulizuka juzi majira ya saa 6.30 mchana katika ghorofa ya tatu ya jengo hilo na kuteketeza vizimba 14 na bidhaa zote zalizokuwemo huko ambapo gharama zake hazikupatikana kutokana na wafanyabiashara hao kutokuwepo katika vizimba vyao.
 
Akizungumza na chanzo cha habari jana, Wakala wa Bima inayotambulika kwa jina la Jovial Insurance Agency, Roze Mapunda, ambaye ni mmoja kati ya wahanga, alisema chanzo cha moto huo kimesababishwa na fundi umeme aliyekuwa akifanya maboresho katika jengo hilo.
 
Mwingine ni Amad Nassoro, anasema walishtushwa na kishindo kikubwa cha mlipuko wa moto huo toka katika ghorofa ya tatu ndipo waliposhirikiana kwa pamoja na kufanikiwa kuuzima bila kusababisha madhara kwa binadamu.
 
Makamu Mwenyekiti wa soko hilo, Gerald Mpagama, alielezea  chanzo cha moto huo kimesababishwa na fundi umeme aliyekuwa akikata nyaya  za umeme kama njia ya kuboresha vizimba hivyo ndipo cheche za  moto zikaruka katika kizimba cha pili na kusababisha moto huo.
 
Alisema licha ya kikosi cha zima moto kupata taarifa na kufika katika  jengo  hilo, lakini wafanyabiashara hao walikuwa wameshafanikiwa kuuzima moto huo wenyewe.
 
 “Elimu ya kikosi cha zima moto kwa wafanyabiashara imetusaidia sana kwani leo (jana), kwa kushirikiana tumefanikiwa kuuzima moto ,” alisema Mpagama.