Stori:  Issa Mnally Na Richard Bukos
OFM kazini! Kile kitengo maarufu cha Global Publishers cha Operesheni Fichua Maovu (OFM) mwishoni mwa wiki kilifanikiwa kunasa tukio la aina yake baada ya kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Joni Simon kunaswa na kitita cha fedha bandia akitaka kuwekewa katika simu yake ya mkononi kupitia mtandao wa Tigo Pesa, tukio lililotokea Sinza Afrika Sana jijini Dar.Mashuhuda waliwaambia OFM kuwa kijana huyo alinaswa katika duka moja la Tigo Pesa lililopo maeneo ya Kona Bar karibu na Hoteli ya kisasa ya Atriums.Baada ya kuwekewa pesa katika simu yake, alitoa ‘mkwanja huo bandia’ na kumkabidhi jamaa wa Tigo Pesa, lakini alizitilia mashaka fedha hizo na kulazimika kumzuia asiondoke kwanza, lakini jamaa huyo akataka kutimua mbio.Kabla hajafanya hivyo, jamaa wa Tigo Pesa alimrukia na kumshika huku akipiga kelele za kuomba msaada ndipo akaupata kutoka kwa wauza chips walio karibu.Ndipo simu ilipopigwa kwa polisi wa kituo cha Mabatini Kijitonyama ambao wakiongozwa na Kamanda Rashidi wakaingia eneo la tukio mara moja lakini walilazimika kutumia bunduki kumtisha ili kumtuliza kijana huyo na kumtia mbaroni.
Baada ya kumpekua walimkuta na kiasi cha zaidi ya shilingi laki mbili, zote zikiwa bandia na waliondoka naye kuelekea kituoni kwa mahojiano zaidi kabla ya hatua nyingine za kisheria kufuata.Tukio hilo limetokea siku chache tu baada ya mtu mmoja huko mkoani Mwanza, kukamatwa akiwa na kiasi cha shilingi milioni 400 za Kitanzania, ambazo pia ni bandia, zilizokusudiwa kuingizwa katika mzunguko wa fedha.