Ndizi zikiwa zimeanguka baada ya mvua kubwa kunyesha
Mbozi. Mvua ya mawe iliyonyesha jana alasiri katika Kijiji cha Isansa, Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya kwa zaidi ya dakika 40, imeezua mabati ya nyumba na kuharibu zaidi ya ekari 300 za mashamba.
Shuhuda wa tukio hilo, Henry Mgalla alisema kuwa mvua hiyo ilianza kunyesha saa 9.20 alasiri.
Alisema hilo ni tukio la kwanza kutokea katika eneo hilo na mawe yenye ukubwa mithili ya tufe, yalidondoka na kujeruhi mifugo.
Mgalla aliiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma katika kutoa msaada kwa waathirika kwani maisha yao yanategemea kilimo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Dk Michael Kadeghe alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa ekari 168 za mashamba ya kahawa, 134 za mahindi na 61.2 za mashamba ya maharagwe zimeharibiwa.
Alisema hakuna mtu aliyejeruhiwa na kwamba tathimini ya uharibifu wa nyumba inaendelea kufanywa.
Ofisa Ugani wa Kata ya Isansa, Christopher Mwansasu alisema kutokana na madhara ya mvua hiyo, hakuna mazao yatakayopatikana kwenye mashamba hayo.
|
0 Comments