Kiungo wa timu ya Yanhga Haruna Nyonzima akiwania mpira na beki wa timu ya BDF ,Othusitse Mpharitlhe  Botswana  wakati wa mchezo uliofanyika katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana.Picha na Said Khamis
Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amisi Tambwe leo ameibuka shujaa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kuifungia timu yake ya Yanga magoli na kuifanya timu hiyo kuibuka na ushindi hu wa 2-0 dhidi ya BDF XI ya nchini Botswana.
Yanga na BDF XI zimekutana leo kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya awali ya kombe la shirikisho la soka barani Afrika.
Wachambuzi wa soka wanaelezea kuwa ushindi huo wa magoli 2-0 unaiweka timu ya Yanga katika nafasi nzuri ya kuweza kuingia hatua ya 32 bora.
Tambwe aliipatia timu yake goli la kwanza katika dakika ya kwanza kwa kichwa akiunganisha  krosi nzuri iliyopigwa na winga machachari Simon Msuva huku mabeki wa BDF XI wakibaki wanashangaa.
Goli hilo lilidumu hadi kipindi cha kwanza ndipo tena Tambwe alipoibuka tena katika dakika ya 55 akiifungia timu yake goli la pili kwa kichwa baada ya kuunganisha krosi nzuri kutoka kwa Mrisho Ngassa.