Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Leo tunakutana tena nikiamini kwamba wasomaji wote wa safu hii hamjambo, Mungu azidi kutuongoza katika njia ya kweli. Ni marufuku kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kujitangaza kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Huo ndiyo mwongozi wa chama tawala ambao nitauchambua hapa.
Ukweli ni kwamba idadi ya wanaotaka kugombea nafasi ya urais inaongezeka siku hadi siku, wengine wanalilia nafasi hiyo na wanataka waipate kwa udi na uvumba, wapo wanaosakiziwa na wengine wanafanya usanii kwa kujifanya kama vile hawataki huku vikundi vikijitokeza kuwaomba wahusika kuchukua fomu muda ukifika na baadhi wakisema kwao kutangaza mpaka waoteshwe!

Imedhihirika kuwa wanaotamani nafasi ya urais ni rundo la watu lakini bahati mbaya ni kwamba nafasi hiyo ni moja kwa mtu mmoja tu.Vyama vya upinzani hakuna zuio la kujitangaza kama ilivyo CCM lakini wanaotaka wanapitapita na wala hawataitwa ‘mahakamani’ kujitetea.
Waliojitokeza CCM na kutangaza nia ya kugombea urais walijikuta wakiwa ‘kifungoni’, baada ya kuitwa kujitetea, hili lilishangaza wengi kwa sababu mwisho wa yote ni watu kujulikana na wapiga kura. Mwaka jana, CCM iliwafungia wanachama wake sita waliojitokeza kujitangaza kugombea urais. Wakapata adhabu ambayo hadi leo ni kama inaendelea maana, hakuna uwazi.
Katika dunia ya leo ya sayansi na teknolojia, bado chama tawala wanataka mambo yaende kimya kimya kama enzi zile za ujima? Siku, zinakwenda na wapiga kura wangependa kuwapima wagombea, pengine na kuwahoji na kuwachunguza uadilifu wao na mambo mbalimbali.
Upo umuhimu wa kumfahamu mtu anayetaka kugombea uongozi wa juu katika taifa, tujue anafuata sera gani? Ni mzalendo au ni kibaraka? Yote haya ni muhimu kufahamika mapema.Wagombea wa CCM ni watu wanaoishi kwenye jamii yetu hivyo chama hicho kilitakiwa mwaka huu kingewaruhusu kujitangaza mapema ili watu wafukunyuefukunyue habari zao kuona kama wanatufaa au laa!
Hakuna ushahidi mpana unaoonyesha kwamba Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM inawafahamu vizuri wagombea wote watakaojitokeza kuwazidi Watanzania wanaoishi nayo mitaani.
Ukweli ni kwamba kama mgombea watu watamjua kuwa ni fisadi au anajulikana kwa kula na kutoa rushwa, kufuja hovyo pesa za umma au ana kiburi na majigambo, anajulikana kwa kutotumikia bali kutumikiwa na si mzalendo, ni wazi atakuwa hafai kutuongoza.
Mtu kama huyo akiibuka kutaka uongozi, Halmashauri Kuu ya CCM haiwezi kuibadilisha hali yake hiyo chafu hata asafishwe kwa brashi ya chuma!Vijana, wengi wamejitokeza na kuonyesha hamu ya kutaka kuliongoza taifa letu. Ni wazi wengine hawana historia hata ya kuandika chochote juu ya maisha yao, lakini wapo ambao wana uwezo mkubwa.
Lakini wapo baadhi ya wagombea wanaoongozwa na tamaa ya madaraka, wengine wanafaa wengine hawafai. Sasa tujiulize kuna ubaya gani mtu kujitangaza kutaka kugombea urais, udiwani au ubunge na wananchi wakamjadili huku wakingoja vikao vya chama?
Akitumia njia mbovu, ukifika wakati wa kura za maoni, ni wazi atatupwa nje. Mimi kama Mtanzania na mzalendo wa kweli, nina lengo la kuwakumbusha vigogo wa CCM kwamba sauti ya watu ni sauti ya Mungu.
 CCM kupitia viongozi wake imesema kwamba mtu mwenye sifa zisizotiliwa shaka ndiye atapeperusha bendera ya chama chao, sasa kwa nini wasifungue milango watu wakapitapita mitaani kutangaza nia?

Hivyo ni muhimu tukawafahamu wagombea wa CCM mapema hasa kwenye urais ili tumpime na kumhoji na yeye ajieleze na kujipima na wagombea wa vyama vingine. Hivi ndivyo nchi zilizoendelea na zile zinazofuata demokrasia zinafanya.Wagombea wanafahamika kwa watu zaidi ya mwaka mzima. Huu mfumo wa kuviziana ni mbinu ya zamani ambayo tunaifanya sisi Watanzania tu!
Baba wa Taifa, Julius Nyerere aliwahi kuwaonya viongozi wa chama tawala kwamba kama kuna mtu anatangaza nia ya uongozi na akawa anabebwa kama jeneza aachwe, kwani wabebaji watambeba mpaka watachoka wenyewe.
Hivyo ni wito wangu kwa CCM, kuwaruhusu wanaotaka kugombea nafasi zote za uongozi kuwaruhusu wajitangaze ili watu wawajuwe, wawatathmini, kama wanavyofanya wagombea wa vyama vingine na kazi iwe kwa wapiga kura kuchagua pumba ni zipi na mchele ni upi.
 
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.