Wanafunzi waandamana Kampala kupinga ugaidi
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda wamefanya maandamano ya mshikamano na wenzao waliofikiwa na mkasa katika chuo kikuu cha Garissa nchini Kenya hivi majuzi.
Wanafunzi hawa wamepiga kwata hadi ubalozi wa Kenya nchini Uganda na kutoa rambi rambi zao.

Wanafunzi hao wa wa chuo kikuu cha Makerere mjini Kampala waliandamana wakisindikizwa na bendi moja huku wakipewa ulinzi na polisi kuelekea ubalozi wa Kenya.
Shambulio dhidi ya Chuo cha Garissa lilisababisha watu 148 kupoteza maisha yao wengi wao 142 wakiwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Garisa .
Kundi la Al Shabaab lilidai kuhusika.
Wanafunzi kutoka Kenya waliimba wimbo wa taifa nje ya ubalozi wao
Mwanafunzi mwingine Naomi Hacho alisema kuwa wanaungana na wenzao waliuawa wakitafuta elimu ilikuboresha maisha yao katika siku za usoni.''
Mbele ya ubalozi huo wa Kenya wanafunzi wengi kutoka Kenya waliimba wimbo wa taifa lao na kutoa risala za rambi rambi kwa wenzao waliaga dunia.
Wanafunzi hao wakiwa na mabango yenye maandishi tofauti lakini yakiwa na mada ya kukashifu mauaji hayo pamoja na ugaidi kwa jumla.
Walihutubiwa na afisa mmoja wa ubalozi huo Kanali Julius Ngera kwa niaba ya balozi Okanga ambaye alikuwa katika shughuli tofauti.
Wanafunzi 142 waliuawa katika chuo kikuu cha Garissa
Maandamano hayo ya amani yaliandaliwa na mkuu wa wanafunzi wa chuo kikuu cha Makerere David Bala ambae miongoni mwa mengine amesema aliwasilisha risala za rambirambi kwa ubalozi wa Kenya.
Alisema kuwa ni wajibu wao kuungana ili kupigana dhidi ya ugaidi na huu ndio mwanzo tu wa safari ndefu ya vita dhidi ya ugaidi.
Aidha alisema kuwa wanafunzi ndio walioibuka kuwa walengwa wa kundi hilo haramu.
Wanafunzi hawa pia wamezindua mikakati ya kukabiliana na tisho la kigaidi katika chuo kikuu cha Makerere.