Skendo? Wakati akiwa na mkataba wa shilingi bilioni nane na nusu wa bidhaa zenye nembo yake kutoka Kampuni ya Rainbow Shell Craft, mwanamitindo maarufu Bongo, Jokate Mwegelo ‘Kidoti’ amekwaa kashfa ya utapeli akidaiwa ‘kuchikichia’ shilingi elfu sabini za msanii wa Bongo Fleva anayefahamika kwa jina la Abdallah Hamis ‘Planet’, Ijumaa Wikienda lina mchapo kamili.
CHANZO CHAANIKA UBUYU
Kwa mujibu wa chanzo makini, Planet alimuomba Jokate ashiriki kama ‘video queen’ kwenye video yake iitwayo Jokate ambapo walipatana kazi hiyo kwa shilingi laki moja na nusu ndipo Planet alipotanguliza kianzio cha shilingi elfu sabini.
“Baada ya makubaliano ya mdomo, Planet alimkabidhi Jokate shilingi elfu sabini kama advance (kianzio) ili atakapomaliza kazi, ammalizie shilingi elfu themanini iliyobaki.
JOKATE KAINGIA MITINI?
“Sasa cha kushangaza, siku waliyopanga kufanya kazi, Jokate hakutokea katika eneo walilokubaliana na hata alipopigiwa simu hakupokea tena ndipo Planet alipoanza kumsaka kila kona bila mafanikio,” kilisema chanzo hicho.
PLANET AFUNGUKA
Baada ya chanzo hicho kumwaga ubuyu huo kwenye meza ya Ijumaa Wikienda, mapaparazi wetu walimvutia waya Planet ambapo alidai kuwa anashindwa kumuelewa Jokate kwa kitendo chake cha kumuingiza mjini.
“Dah! Unajua ile ngoma yangu nimemuimba yeye kwa lengo zuri tu kwa kuwa mimi ni shabiki wake, sasa baada ya kuachia audio nilipofikiria suala la video nikaona bora nimshirikishe awe video queen nikiamini itapendeza zaidi kwa kuwa itakuwa imeonesha uhalisia, nilimwambia akakubali baada ya kuisikiliza na kuipenda.
KUMBE NI TANGU MWAKA JANA
“Mchakato huo ulikuwa tangu mwaka jana mwezi wa tisa na makubaliano yetu alitaka nimpe laki moja na nusu, lakini akaniambia nimpe kianzio shilingi elfu sabini, cha kustajabisha tangu hapo amekuwa akinichenga hata nikipiga simu hapokei pamoja na kwenda nyumbani kwao mara kadhaa kumuulizia lakini huwa haoneshi hata kutaka kunisikiliza natimuliwa na walinzi,” alisema Planet huku akirekodiwa sauti.
AMUIBUKIA NYUMBANI
Ili kutaka kuwaridhisha wanahabari wetu, Planet aliwaomba waende naye nyumbani kwa Jokate, Oysterbay jijini Dar kushuhudia namna ambavyo amekuwa akipigwa chenga kila anapodai chake.
AWEKA KAMBI GETINI
Mapaparazi wetu walipofika nyumbani hapo huku wakipiga picha hatua kwa hatua, walishuhudia Planet ‘akichomeshwa mahindi’ bila geti kufunguliwa licha ya kugonga kwa muda mrefu
JOKATE ADAI YUPO BIZE
Wakati Planet akiwa getini hapo, Jokate aliwasili akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Carina ambapo alishusha kioo na kumwambia msanii huyo kuwa yupo bize amtafute kwa simu.
AINGIA, GETI LAFUNGWA
Baada ya kumwambia maneno hayo, Jokate aliingia ndani kisha walinzi kufunga geti na kumwacha Planet akiwa nje.
JOKATE ANASEMAJE?
Ijumaa Wikienda lilimtafuta Jokate kwa njia ya simu ambapo alipopatikana alijibu kwa kifupi kuwa hamfahamu Planet na kwamba anatafuta umaarufu kupitia jina lake.
“Simfahamu huyo msanii labda anatafuta kiki tu.”
0 Comments