Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika na Mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje  akiwasili katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.
John Mnyika akihutubia wananchi wa Mwanza jana.
Wakazi wa Mwanza wakifuatilia mkutano huo wa uzinduzi wa Kanda ya Ziwa Victoria.

Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiel Wenje akiongea na wananchi wa Mwanza.
Wananchi wakizidi kufuatilia mkutano huo.
Na Johnson James, Mwanza
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Mnyika, jana amezindua rasmi Kanda ya Ziwa Victoria aliposisitiza wananchi wajiandikishe katika daftari la wapiga kura.
Akiwahutubia mamia ya wananchi kwenye uwanja wa Furahisha jijini hapa, amesema kuwa katika kipindi cha uchaguzi mkuu kila mara kumekuwa na tatizo la ndugu zetu Watanzania kufariki katika ajali mbalimbali na serikali hukaa kimya bila kutoa tamko kuhusu ajali hizo.
Mnyika amemtaka Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta, kwa kushirikiana na Rais Kikwete watoe tamko kwa wananchi kuhusu kitu kinachoendelea kusababisha ajali hizi ambapo mamia ya wananchi wameendelea kupoteza maisha yao.
Aidha Mnyika amesema kuwa katika bunge lijalo linalotarajia kuanza mwezi Mei mwaka huu atahakikisha kuwa anaishinikiza serikali ili isipitishe muswaada wa haki ya kupata habari kwani vijana wengi watakosa ajira kutokana na muswada huo kusema kuwa ili uwe mwandishi wa habari lazima uwe na shahada,  jambo ambalo waandishi wengi hapa nchini hawajafikia elimu hiyo kutokana na mazingira wanayotoka.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Nyamagana jijini hapa, Ezekiel Wenje, amesema kuwa ameishangaa serikali kwa kufunga shule kutokana na shule hizo za serikali kukosa chakula huku baadhi ya viongozi katika serikali hii wakiendelea kula pesa za nchi hii bila kujali athari ya elimu kwa vijana walio mashuleni na kuitaka serikali kununua vyakula na kukipeleka katika shule zilizofungwa kwani uwezo wa serikali kununua vyakula hivyo inao.